Michezo

Manangoi achuma nafuu kutokana na Covid-19, sasa alenga dhahabu ya olimpiki

May 28th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADHI ya wanariadha wanapoendelea kukadiria hasara kutokana na janga la corona, bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 1,500 Elijah Manangoi anasalia kuchuma nafuu kutokana na likizo hiyo kadri anavyolenga kujifua zaidi baada ya kupona jeraha.

Manangoi alipata jeraha baya la kifundo cha mguu mnamo 2019 ambalo hatimaye lilimkosesha fursa ya kutetea ubingwa wa dunia katika Riadha za Doha, Qatar.

Ingawa hivyo, Mkenya Timothy Cheruiyot ambaye ni mwenzake katika kambi ya mazoezi na kikosi cha Rongao Athletics Club, alijizolea nishani ya dhahabu katika mbio hizo na kudumisha ufalme huo humu nchini.

Manangoi ambaye pia ni Bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 1,500 alikuwa akipania kurejea ulingoni mnamo Aprili wakati wa mbio za Wanda Diamond League.

Riadha hizo ambazo Manangoi amesema zitampa majukwaa mwafaka zaidi ya kujifua kwa Olimpiki za Tokyo nchini Japan mwaka ujao, kwa sasa zimeahirishwa hadi Agosti 2020.

Huku wengine wakisikitikia likizo ndefu ya lazima kutokana na corona, Manangoi anashikilia kwamba hiyo imempa fursa ya kupona na kujiandaa vilivyo kwa kampeni za msimu huu zitakazoanza jijini Turku, Finland mnamo Agosti 2020.

“Nilikuwa naharakisha kupona kwa minajili ya duru ya kwanza ya Diamond League jijini Doha lakini ujio wa corona na hatimaye likizo ndefu katika kalenda ya riadha zimenipa wakati maridhawa zaidi za kupona na kujifua vilivyo kwa vibarua vilivyopo mbele yangu. Sasa niko sawa na tayari kunogesha mbio za Diamond League zitakazorejelewa jijini Monaco, Ufaransa mwishoni mwa Agosti.”

Ingawa kubwa zaidi katika maazimio ya Manangoi ni kutwaa medali ya dhahabu katika Olimpiki zijazo, ameshikilia kwamba kushiriki kwake Diamond League kutamnoa ipasavyo kwa michezo hiyo. Jeraha lilimhini Manangoi fursa ya kushiriki Olimpiki za Rio 2016 nchini Brazil.

Kwa sasa Manangoi ni miongoni mwa wanariadha watano wa Rongai Athletics Club wanaojiandaa kwa mbio za Maurie Plant Memorial zitakazoandaliwa uwanjani Nyayo mnamo Juni 11.

Wawili kati ya wenzake hao ni Cheruiyot na bingwa wa kitaifa katika mbio za mita 800, Edwin Melly.

Cheruiyot ambaye ni mshikilizi wa taji la Diamond Trophy aliambulia nafasi ya pili nyuma ya Manangoi katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

“Nimerejea ulingoni nikitawaliwa na kiu kubwa ya kutawala mbio zijazo za Diamond League na hatimaye kutwaa dhahabu katika Olimpiki. Nishani ya Olimpiki ndiyo ya pekee inayokosekana katika kabati langu la medali. Hii ni ndoto ambayo naomba sana itimie,” akasema Manangoi.