Michezo

Manangoi kutumia mbio za Maurie Plant kupima uwezo wake wa kuwika Diamond League na Olimpiki

June 9th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa zamani wa dunia katika mbio za mita 1,500 Elijah Manangoi amesema atatumia mbio zijazo za Maurie Plant Memorial kujipima kiwango cha maandalizi yake kwa kampeni atakazozishiriki msimu huu.

Riadha za Maurie zitakazowashirikisha pia Timothy Cheruiyot aliyeibuka bingwa wa dunia katika mita 1,500 mnamo 2019 na Edwin Melly wa mbio za mita 800, zitaandaliwa katika uwanja wa Nyayo mnamo Juni 11, 2020.

Manangoi anarejea ulingoni baada ya jeraha la goti kumweka nje ya Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar alikotarajiwa kutetea ufalme wake.

Manangoi ambaye pia ni Bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 1,500, atapania vilevile kunogesha mbio za Wanda Diamond League mnamo Agosti 2020.

Riadha hizo ambazo Manangoi amesema zitampa majukwaa mwafaka zaidi ya kujifua kwa Olimpiki za Tokyo nchini Japan mwaka ujao, kwa sasa ziliahirishwa kutoka Aprili 2020.

“Nilikuwa naharakisha kupona kwa minajili ya duru ya kwanza ya Diamond League jijini Doha lakini ujio wa corona na hatimaye likizo ndefu katika kalenda ya riadha zimenipa wakati maridhawa zaidi za kupona na kujifua vilivyo kwa vibarua vilivyopo mbele yangu. Sasa niko sawa na tayari kunogesha mbio za Maurie kisha Diamond League zitakazorejelewa jijini Monaco, Ufaransa mwishoni mwa Agosti,” akasema.

Ingawa kubwa zaidi katika maazimio ya Manangoi ni kutwaa medali ya dhahabu katika Olimpiki zijazo, ameshikilia kwamba kushiriki kwake Diamond League kutamnoa ipasavyo kwa michezo hiyo. Jeraha lilimnyima Manangoi fursa nyingine ya kushiriki Olimpiki za Rio 2016 nchini Brazil.

Manangoi kwa sasa ni miongoni mwa wanariadha watano wa Rongai Athletics Club wanaojiandaa kwa mbio za Maurie Plant Memorial.

Cheruiyot ambaye ni mshikilizi wa taji la Diamond Trophy aliambulia nafasi ya pili nyuma ya Manangoi katika Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.

“Nishani ya Olimpiki ndiyo ya pekee inayokosekana katika kabati langu la medali. Hii ni ndoto ambayo naomba sana itimie sana mwakani,” akasema Manangoi.