Michezo

Manchester City kukosa Rodri gozi na Aston Villa

October 26th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER City wataingia uwanjani leo Jumamosi kucheza na Aston Villa bila kiungo mahiri Rodri anayeuguza jeraha la paja, pamoja na Oleksandr Zinchenko, lakini huenda beki John Stones akarejea tangu aumie Septemba.

Kwa upande mwingine, Villa watamkaribisha James Chester ambaye hajacheza tangu msimu uanze, kadhalika Jonathan Kodjia na Kortney Hause wanatarajiwa kurejea baada ya kukaa nje kwa muda mrefu.

Mchezaji pekee atakayekosekana kikosini ni Jota anayeendelea kuuguza jeraha linalomsumbua chini ya tumbo.

Manchester City wanajivunia ushindi mara tisa katika ligi kuu ya Uingereza (EPL) pamoja na asilimia kubwa ya mabao dhidi ya Aston Villa.

Vijana hao wa kocha Pep Guardiola hawajapoteza nyumbani tangu Februari 2007 waliposhindwa na Reading FC, na pia itakumbukwa Sergio Aguero amefunga mabao sita langoni mwa Aston Villa katika mechi nne zikiwemo ugani Etihad.

Gabriel Jesus amefunga mabao saba mfululizo kila alipopewa nafasi ya kuanza mechi, huku kikosi hicho pia kikijivunia uwepo wa mshambuliaji Raheem Sterling anayeongoza kwa ufungaji mabao msimu huu baada ya kupachika wavuni 12 katika mechi 13.

Wakati huo huo, mechi ya leo Jumamosi itakuwa ya 200 kwa Fernandinho katika ligi kuu ya EPL ambaye siku hizi anapangiwa katika safu ya ulinzi kufuatia kuumia kwa mabeki muhimu wa kikosi hicho.

Villa watakuwa wakiwania ushindi wa tatu mfululizo wa EPL tangu Aprili 2010, walipokuwa chini ya kocha Martin O’Neill.

Kuendeleza ubabe

Kwingineko, kocha Frank Lampard atakuwa akilenga kuhakikisha vijana wake wameendeleza ubabe wao watakapokuwa ugenini kukabiliana na Burnley.

Chelsea wanaingia uwanjani baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Amsterdam Ajax kwenye mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Ushindi huo ulikuwa ya nne mfululizo kwa Chelsea ugenini, baada ya hapo awali kuandikisha ushindi dhidi ya Wolverhampton Wanderers, Lille na Southampton.

Lampard ameeleza kuridhika kwake na uelewano kikosini huku akitarajia vijana wake kuimarika zaidi, huku akiwasifu Christian Pulisic na Michy Batshuayi baada ya viwango vyao kupanda.

Awali, Pulisic alikuwa hapewi nafasi ya kuanza mechi, lakini ameanza kutambuliwa na Lampard baada ya majuzi nyota huyo kuchangia katika mabao ya ushindi yaliyopatikana dhidi ya Newcastle United na baadaye Ajax.

Batshuayi, kwa upande wake amekuwa akiiongezea nguvu safu ya ushambuliaji kila apewapo nafasi; vile vile ndiye aliyefunga bao la ushindi jijini Amsterdam majuzi.