Manchester City kumsajili beki Sergio Ramos iwapo Real Madrid watakataa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili

Manchester City kumsajili beki Sergio Ramos iwapo Real Madrid watakataa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City wameanza mazungumzo ya kumshawishi beki Sergio Ramos kujiunga nao muhula huu wa uhamisho wa wachezaji iwapo Real Madrid hawatakuwa radhi kurefusha mkataba wake ugani Santiago Bernabeu.

Nahodha huyo wa Real amesitisha mchakato wa kujadiliana na Real kuhusu kandarasi mpya baada ya ile aliyo nayo kwa sasa kambini mwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kutamatika Juni 30, 2021.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City wanalenga kuimarisha uthabiti wa safu yao ya ulinzi ambayo kwa sasa inajivunia huduma za Ruben Dias, 23, Nathan Ake, 25, John Stones na Aymeric Laporte ambao wana umri wa miaka 26 kila mmoja.

Dias aliingia katika sajili rasmi ya Man-City mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21 baada ya kukatiza uhusiano na Benfica ya Ligi Kuu ya Ureno mnamo Septemba.

“Tunahitaji beki veterani ambaye ataleta uzoefu mpana na tajriba pevu itakayoboresha kikosi katika idara ya ulinzi. Ramos anajivunia sifa hizo. Ataleta pia sifa za uongozi na ataamsha viwango vya ushindani miongoni mwa chipukizi tulio nao,” akasema Guardiola kwa kukiri kwamba amekuwa akimvizia beki huyo raia wa Uhispania kwa kipindi kirefu.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Real wako radhi kumpokeza Ramos mkataba wa mwaka mmoja japo sogora atakayefikisha umri wa miaka 35 mnamo Machi 2021, amekuwa akitaka muda wake wa kuhudumu ugani Bernabeu kurefushwa kwa miezi 24 zaidi.

You can share this post!

Spurs wakomoa Brentford 2-0 na kufuzu kwa fainali ya...

ODM wahofia Jubilee inakoroga Raila