Manchester City kumsajili Griezmann iwapo mpango wao wa kujinasia Harry Kane utatibuka

Manchester City kumsajili Griezmann iwapo mpango wao wa kujinasia Harry Kane utatibuka

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City wamefichua azma ya kumshawishi Antoine Griezmann kujiunga nao iwapo juhudi za mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumsajili Harry Kane kutoka Tottenham Hotspur zitazaa nunge.

Ingawa yalikuwa matamanio ya Man-City kumtwaa Kane ambaye aliwaeleza waajiri wake kuhusu nia yake ya kuhamia kwingine mnamo Mei 2021, matumaini hayo yanazidi kudidimia.

Hii ni baada ya Kane kufichua kwamba asingetaka majadiliano yoyote kwa sasa kuhusu mustakabali wake kitaaluma ikizingatiwa kwamba kubwa zaidi katika mpango wake ni kuongoza Uingereza kutia kapuni ubingwa wa Euro.

Msimamo huo unakinzana na wa kocha Pep Guardiola ambaye anataka kukisuka mapema kikosi chake na kuanza maandalizi ya msimu mpya mara moja akijivunia wanasoka wote wa zamani pamoja na sajili wapya.

Licha ya Man-City kuwasilisha ofa mpya ya Sh15.6 bilioni kwa ajili ya kushawishi Tottenham kumwachilia Kane atue ugani Etihad, mwenyekiti Daniel Levy amesisitiza kwamba kikosi chochote kinachomezea mate huduma za Kane kina ulazima wa kuweka mezani kima cha Sh23 bilioni. Aidha, ameshikilia kuwa Tottenham hawako radhi kushuhudia Kane akijiunga na washindani wao wakuu kwenye EPL.

Kane ni miongoni mwa washambuliaji wawili akiwemo Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund ambao wanaviziwa na kocha Guardiola kwa malengo ya kujaza pengo la Sergio Aguero aliyeyoyomea Barcelona.

Hata hivyo, Dortmund wamesisitiza kwamba hawana nia ya kumtia Haaland mnadani ikizingatiwa kwamba wako radhi kuagana na Jason Sancho anayemezewa mate na Manchester United.

Kane anahamu kuondoka Spurs, kikosi ambacho amekiwajibikia tangu akiwa mwanafunzi.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror Sport, Man-City wako tayari kujiondoa katika vita vya kufukuzia maarifa ya Kane iwapo Spurs watakataa fedha ambazo wameziweka mezani.

Iwapo mpango huo utafikia hatua hiyo ya kutibuka, Man-City watamvizia Griezmann kwa matarajio kwamba atakuwa radhi kuondoka Barcelona baada ya miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kujinasia maarifa ya Aguero. Mchezaji mwingine anayehemewa na Man-City ni nyota wa Southampton, Danny Ings.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mpango wa Crystal Palace kuajiri kocha Lucien Favre wagonga...

Wanafunzi 30 wapokea ufadhili kutoka kwa MKU