Manchester City roho juu ikiwaalika Southampton leo Jumatano kwa gozi la EPL ugani Etihad

Manchester City roho juu ikiwaalika Southampton leo Jumatano kwa gozi la EPL ugani Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City watakuwa leo wenyeji wa Southampton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) inayotarajiwa kuwapa jukwaa mwafaka la kujinyanyua baada ya Manchester United kuwapapetea 2-0 mnamo Machi 7, 2021.

Mchuano huo utatandaziwa uwanjani Etihad kuanzia saa tatu usiku.

Kichapo hicho kutoka kwa Man-United kilipiga breki rekodi nzuri iliyoshuhudia masogora hao wa kocha Pep Guardiola wakishinda jumla ya mechi 21 mfululizo.

Hata hivyo, wangali wanajivunia pengo la alama 11 kileleni mwa jedwalini na ushindi katika gozi la leo utawawezesha kufungua mwanya wa pointi 14 zaidi kati yao na Man-United wanaoshikilia nafasi ya pili kwa alama 54.

Kwa upande wao, Southampton watajibwaga ugani wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 dhidi ya Sheffield United katika mechi iliyopita ugani Bramall Lane. Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Southampton kusajili kutokana na mechi 10 za hivi majuzi ligini.

Chini ya kocha Ralph Hassenhutl, Southampton kwa sasa wanashikilia nafasi ya 14 kwa alama 33 na ni pengo la pointi saba pekee ndilo linawatenganisha na nambari 18, Fulham.

West Bromwich Albion, Sheffield United na Fulham ni miongoni mwa vikosi vitatu vinavyokodolea macho hatari ya kuteremshwa daraja kwenye EPL msimu huu.

Ushirikiano mkubwa kati ya Bruno Fernandes, Anthony Martial na Luke Shaw uliwawezesha Man-United kuangusha Man-City wikendi iliyopita. Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kwa wanasoka hao wa Guardiola kupoteza baada ya kutoshindwa katika jumla ya michuano 28 ya awali tangu Novemba 2020.

Mbali na kufukuzia taji la EPL msimu huu, masogora wa Guardiola wangali kwenye mawindo ya ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la FA na ubingwa wa EFL League Cup.

Kikubwa zaidi kinachotarajiwa kuwapa motisha wachezaji wa Man-City leo ni msukumo wa kutaka kutoshindwa katika mechi mbili mfululizo ligini kwa mara ya kwanza tangu Februari 2016.

Guardiola hajawahi kushindwa nyumbani kwenye mechi mbili mfululizo za ligi katika kipindi kizima cha ukufunzi wake.

Southampton wamepoteza mechi nane kati ya tisa zilizopita dhidi ya Man-City ligini katika uwanja wa Etihad. Ushindi wa pekee uliowahi kusajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Man-City ugenini ni Aprili 2004.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Klopp afutilia mbali uwezekano wa kuwa kocha mpya wa timu...

Page kuendelea kutekeleza majukumu ya kocha Ryan Giggs...