Michezo

Manchester City wala sare ya 1-1 na West Ham katika EPL

October 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MICHAIL Antonio alifunga bao na kuwasaidia West Ham kuondoka uwanjani London Stadium na alama moja muhimu kutokana na sare ya 1-1 waliyolazimishia Manchester City katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 24, 2020.

Bao lililofungwa na Antonio kwa ustadi mkubwa baada ya kushirikiana na Vladimir Coufal katika dakika ya 18 liliwaweka West Ham kifua mbele na likatosha kuwapa alama ya nane kutokana na mechi nne zilizopita.

Kikosi hicho cha kocha David Moyes kilijibwaga ugani baada ya kutoka nyuma na kusajili sare ya 3-3 dhidi ya Tottenham wikendi iliyopita. Awali, kilikuwa kimevuna ushindi wa 4-0 na 3-0 dhidi ya Wolves na Leicester City.

Hata hivyo, chipukizi Phil Foden alitokea benchi mwanzoni mwa kipindi cha pili na kusawazisha mambo katika dakika ya 51 baada ya kupokezwa krosi safi na Joao Cancelo.

Man-City walitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Licha ya kumweka ugani kiungo Kevin de Bruyne aliyekosa mechi mbili za awali za Man-City kutokana na jeraha, masogora wa kocha Pep Guardiola walishindwa kuwazidi maarifa wenyeji wao.

Matokeo hayo yalisaza Man-City katika nafasi ya 11 kwa alama nane sawa na West Ham na Tottenham Hotspur watakaokuwa wageni wa Burnley uwanjani Turf Moor mnamo Oktoba 26, 2020. Man-City wamesajili ushindi mara mbili, kuambulia sare mara mbili na kupoteza mchuano mmoja kati ya mitano ya hadi kufikia sasa kwenye EPL msimu huu.

Kikosi hicho kwa sasa kinajiandaa kuwaendea Olympique Marseille kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 27, 2020 nchini Ufaransa kabla ya kushuka dimbani kwa mechi ya EPL dhidi ya Sheffield United.

Baada ya kuchuana na Olympiacos ya Uturuki kwenye UEFA mnamo Novemba 3, Man-City watakuwa na kibarua kizito cha EPL dhidi ya Liverpool na Tottenham kwa usanjari huo. Kwa upande wao, West Ham wana wiki nzima kujiandaa kwa gozi kali dhidi ya Liverpool mnamo Oktoba 31, 2020 uwanjani Anfield.