Michezo

Manchester City waponda Burnley na kuchelewesha zaidi sherehe ya Liverpool

June 23rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

PHIL Foden na Riyad Mahrez walifunga mabao mawili kila mmoja na kuchangia ushindi mnono wa 5-0 uliosajiliwa na Manchester City dhidi ya Burnley katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 22, 2020 uwanjani Etihad.

Ushindi huo wa Man-City ulichelewesha zaidi sherehe za Liverpool ambao wanatazamiwa kutawazwa mabingwa wa soka ya Uingereza msimu kwa mara ya kwanza baada ya miongo mitatu.

Foden aliwafungulia Man-City karamu ya mabao kunako dakika ya 22 kabla ya Mahrez kuongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Mahrez ambaye ni mzawa wa Algeria, aliongeza goli la tatu la Man-City mwanzoni mwa kipindi cha pili kupitia penalti iliyokuwa zao la fowadi Sergio Aguero kuchezewa visivyo na Ben Mee.

Ushirikiano mkubwa kati ya Foden na Bernardo Silva ulichangia bao la nne lililofumwa wavuni na nahodha David Silva atakayebanduka rasmi uwanjani Etihad mwishoni mwa muhula huu.

Foden alikizamisha kabisa chombo cha Burnley kunako dakika ya 63 baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi aliyomegewa na Gabriel Jesus.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City kwa sasa wanajivunia alama 63 huku pengo la pointi 20 likitamalaki kati yao na viongozi Liverpool. Zimesalia mechi nane pekee kwa kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi.

Iwapo Man-City wangalizidiwa maarifa na Burnley, basi Liverpool wangalihitaji kusajili ushindi dhidi ya Crystal Palace mnamo Juni 24 uwanjani Anfield na kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu.

Badala yake, Liverpool kwa sasa watakuwa na ulazima wa kupiga Palace na kutarajia kwamba Man-City watapoteza alama dhidi ya Chelsea mnamo Juni 25 ili kunyakua ufalme wa EPL kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Man-City uwanjani Etihad mnamo Julai 2.

Man-City ambao tayari wametia kapuni ubingwa wa Carabao Cup, sasa wanafukuzia fursa ya kutetea Kombe la FA na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza katika historia.

Burnley kwa sasa wamepokezwa vichapo vya 5-0 kutoka kwa Man-City katika jumla ya michuano mitatu iliyopita uwanjani Etihad. Kikosi hicho cha kocha Sean Dyche kwa sasa kinajiandaa kuvaana na Watford uwanjani Turf Moor mnamo Juni 25.