Michezo

Manchester City waponea adhabu baada ya CAS kubatilisha maamuzi ya Uefa

July 13th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

IMEKUWA afueni kubwa kwa Manchester City baada ya mahakama ya kimataifa ya mizozo ya spoti (CAS) kubatilisha maamuzi ya awali ya Uefa ambao walikuwa wamewapiga miamba hao wa soka Uingereza marufuku ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kipindi cha misimu miwili.

Kwa mujibu wa CAS, hapakuwepo na ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha matumizi mabaya ya fedha kambini mwa kikosi cha Man-City.

Mnamo Februari 2020 Bodi ya Uefa inayodhibiti matumizi ya fedha miongoni mwa klabu za bara Ulaya (CFCB) iliwaadhibu Man-City kwa kukiuka kanuni za matumizi ya fedha (FFP) kati ya mwaka 2012 na 2016. CFCB pia walidai kuwa Man-City walikataa kushirikiana vilivyo na vinara wa Uefa waliokuwa wakiwachunguza kuhusiana na kesi hiyo.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Man-City, Ferran Soriano alikana madai hayo na kukata rufaa na kesi hiyo ikasikilizwa na mawakili watatu wa CAS kupitia njia ya video za siri kati ya Juni 8-10, 2020.

Mbali na marufuku, Uefa iliwatoza pia Man-City faini ya Sh3.5 bilioni. CAS kwa sasa imepunguza faini hiyo hadi Sh1.2 bilioni pekee baada ya kupata kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola na hatia ya kutatiza uchunguzi dhidi yao walipokosa kushirikiana vilivyo na vinara wa Uefa.

Katika rufaa yao, Man-City walishikilia kwamba maamuzi ya CFCB yalitegemezwa kwa ushahidi uliovujishwa mitandaoni kisiri na ambao haukuwa wa kweli na haki.

“Kasoro nyingi na udhaifu mkubwa ulikuwepo katika mchakato wa uchunguzi wa Uefa. Hakukuwa na shaka kwamba matokeo ya uchunguzi huu yangeishia kuwa hivi: maamuzi yao kubatilishwa na CAS. Kesi dhidi yetu iliyowasilishwa na Uefa, ikashtakiwa na Uefa na aliyetoa uamuzi ni Uefa. Kwa mchakato wa kibaguzi aina hiyo, ilitulazimu kutafuta hukumu ya waamuzi wasiopendelea upande wowote haraka iwezekanavyo. Ni nafuu kubwa kwamba tumepata haki,” akasema Sorriano.

Iwapo marufuku dhidi ya miamba hao wa soka ya Uingereza yangedumishwa, Man-City wasingekuwa sehemu ya vikosi ambavyo vingenogesha kampeni za kuwania ubingwa wa UEFA msimu ujao hata iwapo wangenyanyua ufalme wa kipute hicho muhula huu. Isitoshe, wangezuiliwa kushiriki kivumbi cha Uefa Super Cup mwanzoni mwa msimu ujao dhidi ya mshindi wa Europa League muhula huu.

Tangu atue Etihad mnamo 2016, Guardiola anajivunia kuwashindia Man-City mataji matano yakiwemo mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo miamba hao waliyanyanyua mnamo 2017-18 na 2018-19.

Baada ya kuhifadhi ufalme wa League Cup msimu huu, bado wanafukuzia ubingwa wa Kombe la FA na ufalme wa UEFA. Wao na Bayern Munich kutoka Ujerumani ndio wanaopigiwa upatu wa kutia kapuni taji la soka ya bara Ulaya muhula huu.

Huku Man-City wakisherehekea maamuzi ya CAS, Rais wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) Javier Tebas, amekashifu pakubwa mahakama hiyo.

“Adhabu kwa Man-City ingehakikisha kwamba kuna utekelezaji wa sheria ya kudhibiti matumizi ya fedha na kutoa jukwaa la kunyooshwa vilivyo kwa wanaokiuka sheria hiyo. Yasikitisha kwamba CAS wamekwepa kutoa mwongozo bora kwa mpira wa kandanda ambao kwa sasa unatawaliwa na ulaghai,” akatanguliza.

“Kwa miaka mingi, tumekuwa tukitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua mwafaka dhidi ya klabu za Man-City na Paris Saint-Germain (PSG), na ni ajabu kwamba CAS wameogopa kutoa mfano bora. Ni matumaini yetu kwamba mambo haya ya CAS yatachunguzwa pia. Ni heri kuchelewa kuliko kutochukuliwa kabisa kwa hatua yoyote,” akasisitiza Tebas.