Michezo

Manchester City wasuka njama kuzamisha Spurs

April 17th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

TOTTENHAM Hotspur leo Jumatano usiku watazuru uwanjani Etihad kukabiliana na Manchester City katika mechi ya mkondo wa pili ya kupigania tikiti ya kufuzu kwa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Wenyeji wataingia uwanjani wakilenga kubatilisha matokeo ya kichapo cha 1-0 walichopokea katika mechi iliyochezewa Tottenham Hotspur Stadium, juma lililopita.

Son Heung-min aliyefunga bao la ushindi anatarajiwa kuongoza kikosi hicho cha Mauricio Pottchetino ambacho kitacheza bila nahodha Harry Kane aliyeumia kwenye pambano la awali.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu, imebainika kwamba huenda Kane akakaa nje hadi msimu umalizike.

Golikipa Hugo Lloris wa Tottenham Hotspur afanya mazoezi Aprili 16, 2019, uwanjani Etihad. Picha/ AFP

City ambao wanalenga kutwaa mataji manne msimu huu, wanatarajiwa kuteremsha uwanjani kikosi kikali wakilenga kuendeleza ubabe wao mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Hata hivyo, haijulikani iwapo nyota wao, Fabian Delph na Fernandinho watakuwa kikosini.

Wawili hao walicheza mechi ya mkondo wa kwanza, lakini hawakuwa kikosini Jumapiuli kucheza mechi ya EPL dhidi ya Crystal Palace.

Guardiola aliwashangaza mashabiki alipoamua kuanza na Riyad Mahrez katika pambano hilo badala ya Mjerumani Leroy Sane.

Hata hivyo, Sane alivuma kwenye mechi hiyo iliyochezewa ugani Selhurst Park ambapo alikuwa miongoni mwa waliofunga mabao katika ushindi wao wa 3-1. Staa huyo mwenye umri wa miaka 23 alifunga bao baada ya kuandaliwa pasi na Raheen Sterling.

Kocha Pochettinho anatarajiwa kumpa nafasi Son kuongoza mashambulizi badala ya Lucas Maoura aliyefunga mabao matatu kwenye ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Huddersfield, lakini Dele Alli ataendelea kusubiri hadi atakapopata nafuu kutokana na jeraha.

Timu hizo zitakutana tena hapo Jumamosi katika mechi ya EPL. Ushindi wa Tottenham katika mkondo wa kwanza wa UEFA ulikuwa wa kwanza katika mechi tano baina ya timu hizo, ambapo City wanajivunia ushindi mara tatu.

Zilikutana kwa mara ya mwisho ugani Etihad mnamo Disemba 2017, ambapo City walijipatia ushindi mkubwa wa 4-1, ushindi kama huo utawezesha kutinga nusu-fainali.

Timu zote zina historia sawa, kila moja ikijivunia ushindi mara 61 huku mechi 35 zikimalizika kwa sare.

Kichapo cha majuzi cha 1-0 kutoka kwa Spurs kilikuwa mshtuko kwa wengi ambao wamezoea kuona City wakiwalemea katika mechi za karibuni.

Matumaini

Licha ya kushindwa katika mkondo wa kwanza, City wanawekewa matumaini makubwa ya kushinda na kusonga mbele.

Vijana hao wa Guardiola wanatarajiwa kucheza kwa uangalifu mkubwa huku wakizuia wageni kupenya ngome yao.

Kwa upande mwingine, Spurs wanafahamu bao moja la mapema litawaongezea matumaini ya kushinda na kufuzu kwa nusu-fainali.

Spurs wanatarajiwa kucheza kwa kukaba washambuliaji matata wa City ambao hufunga mabao kupita kiasi.

Ni mechi inayotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa, kwa vile pande zote zinatarajiwa kuwakilisha vikosi imara. Itakuwa vigumu kwa City kushindwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, na wengi wanaitarajia mechi hii ikamalizika kwa 2-0.

Vikosi

Manchester City: Ederson; Walker, Stones, Laporte, Delph; Fernandinho, Silva, Bernardo; Sterling, Sane na Aguero.
Tottenham: Lloris; Trippier, Alderweireld, Vertonghen, Rose; Sissoko, Winks, Eriksen; Alli, Son na Moura.