Manchester City watoka nyuma na kuwazamisha FC Porto kwenye UEFA ugani Etihad

Manchester City watoka nyuma na kuwazamisha FC Porto kwenye UEFA ugani Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walianza vyema kuwinda taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika jaribio lao la 10 kwa kuwapokeza FC Porto kutoka Ureno kichapo cha 3-1 mnamo Oktoba 21, 2020 ugani Etihad.

Licha ya Porto kuchukua uongozi wa mapema kupitia kwa Ruben Luis Diaz katika dakika ya 14, Man-City walirejea mchezoni haraka kupitia penalti ya fowadi Sergio Aguero kabla ya kufungiwa mabao mengine kupitia kwa Ilkay Gundogan na sajili mpya Ferran Torres.

Hadi Diaz alipowafungia Porto, Man-City ya kocha Pep Guradiola haikuwa imeelekeza mpira wowote langoni mwa wageni wao. Goli hilo la Diaz lilichangiwa na Matheus Uribe aliyeshirikiana naye ipasavyo kabla ya kumwacha hoi beki Ruben Dias aliyetua ugani Etihad muhula huu.

Penalti ya Man-City ambayo nusura ipanguliwe na kipa Agustin Marchesin katika dakika ya 20 ilimpa Aguero kupachika wavuni bao lake la 40 katika soka ya UEFA.

Sergio Oliveira nusura awafungie Porto bao la pili mwishoni mwa kipindi cha pili ila akanyimwa fursa hiyo na beki Kyle Walker aliyeondoa mpira kwenye mstari wa goli la Man-City. Man-City walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo siku 67 tangu wabanduliwe na Olympique Lyon ya Ufaransa kwenye robo-fainai za msimu wa 2019-20.

Pigo la pekee kwa Man-City ni jeraha ambalo kwa sasa linatarajiwa kumweka nje kiungo Fernandinho kwa kipindi cha wiki sita zijazo.

Anakuwa mchezaji wa sita wa Man-City baada ya Kevin de Bruyne, Gabriel Jesus, Nathan Ake, Benjamin Mendy na Aymeric Laporte kupata jeraha ambalo litamweka mkekani kwa kipindi kirefu.

Ingawa kanuni za Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) zinakubalia vikosi kupanga wanasoka 12 wa akiba kwenye benchi, Man-City walilazimika kutia kwenye orodha makipa wawili – Zack Steffen na Scott Carson ili kutimiza sheria hiyo.

Man-City watavaana na Olympique Marseille ya Ufaransa katika mchuano ujao wa UEFA katika Kundi C huku Porto wakialika Olympiakos ya Uturuki ugani Do Dragao siku hiyo hiyo ya Oktoba 27, 2020.

Kabla ya hapo, Man-City watakuwa wamevaana na West Ham United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani London Stadium mnamo Oktoba 24.

You can share this post!

Bei jumla ya maski yapanda – wafanyabiashra

Bayern waanza kutetea ufalme wa UEFA kwa kuponda Atletico...