Manchester City wazidisha masaibu ya Arsenal katika EPL

Manchester City wazidisha masaibu ya Arsenal katika EPL

Na MASHIRIKA

MASAIBU ya Arsenal katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu yameendelea baada ya kupokezwa kichapo kinono cha 5-0 kutoka kwa mabingwa watetezi, Manchester City ugani Etihad, Jumamosi.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal ambao ni mabingwa mara tatu wa EPL kwa sasa wamepoteza mechi zote tatu za kwanza muhula huu. Wamefungwa jumla ya mabao tisa na hawana goli wala alama yoyote.

Ilkay Gundogan, Ferran Torres na Gabriel Jesus walifunga mabao ya Man-City katika kipindi cha kwanza kilichoshuhudia kiungo mkabaji wa Arsenal, Granit Xhaka ambaye ni raia wa Uswisi akionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea visivyo Joao Cancelo.

Rodri Hernandez alifunga bao la nne la Man-City katika dakika ya 53 kabla ya Torres kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao dakika sita kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Ilikuwa mara ya tatu mfululizo kwa Man-City kusajili ushindi wa 5-0 katika EPL katika uwanja wao wa nyumbani wa Etihad. Walifunga kampeni za msimu wa 2020-21 kwa kutandika Everton 5-0 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Norwich City wikendi iliyopita, wiki moja baada ya kutandikwa 1-0 na Tottenham Hotspur katika mechi ya kwanza muhula huu.

Arsenal kwa sasa wako ndani ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho kwa mara ya kwanza tangu Agosti 1992 na wanakodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi kwenye EPL kwa mara ya kwanza tangu waanze kunogesha kipute hicho mnamo 1919.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

West Ham wamtwaa beki Kurt Zouma kutoka Chelsea kwa Sh3.9...

Kabras na KCB watinga fainali ya raga ya Kenya Cup baada ya...