Michezo

Manchester United darasani kwa mtihani dhidi ya Burnley

April 27th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI 

MASHABIKI wa Arsenal na Chelsea nchini wameunda muungano wa kushabikia timu ya Burnley ikivaana na Manchester United kuanzia saa 11 jioni uwanjani Old Trafford.

Mtanange huo wa Ligi kuu ya Uingereza (EPL) unatarajiwa kuwa wa kufa kupona ambapo Burnley iliyo katika nafasi ya 19 ikisaka kujinusuru shoka la kushushwa daraja.

Burnley iko na pointi 23 ikiwa imesalia na mechi nne itamatishe ligi lakini ikishinda mtanange wa Jumamosi–ikitarajia walio juu yao watajikwaa–basi itapanda hadi nafasi ya 17 katika jedwali.

Watakaomaliza katika katika nafasi za 18, 19 na 20 ndio watashuka ili kupisha timu nyingine tatu ambazo zitapandishwa ngazi.

Kwa mujibu wa mshirikishi wa mashabiki wa Arsenal mjini Karatina ulioko Kaunti ya Nyeri Bw Simon Muraya, anaunga mkono Burnley “sio kwa sababu nyingine bali tu ni ule uchochezi wa utani wa kispoti”.

“Kimoyomoyo mimi ninajua kwamba huenda Burnley iadhibiwe na Man U lakini kwa chocha zetu, nawatakia hao Mashetani Wekundu, yaani Man U kichapo cha ajabu… ikiwezekana wabebeshwe magoli kwa gunia,” akasema shabiki.

Alisema kwamba ule wakati anaowatakia mashabiki wa Man U kuamka sio kushangilia mabao lakini iwe ni wakiamka kuelekea nyumbani na mikono tu wainue wakipiga mpira wa kona.

Kwa mujibu wa mashabiki wa Chelsea katika mtaa huo wa Karatina, siasa zao za kuunga mkono Burnley zinatokana na msukumamo ulioko katika ari ya kumaliza ligi ndani ya nafasi saba za kwanza.

Timu hizo zote mbili zikiwa hazina matumaini ya kucheza katika dimba la Klabu Bora Barani Ulaya (UEFA) ambalo huchezwa na timu nne za kwanza katika ligi za Ulaya, matumaini ya Man U na Chelsea ni kumaliza katika nafasi za hadi Saba ili kujipa nafasi katika ligi ndogo ya kombe la Europa.

Kwa sasa, timu ya Chelsea iko katika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 47 huku nayo Man U ikiwa katika nafasi ya sita kwa pointi 53.

“Hata hivyo, Chelsea hawajacheza mechi mbili na ambazo ikizishinda itapaa hadi nafasi ya sita ikiwa na pointi 53 na bora tu Man U walimwe leo na Burnley, itakuwa katika nafasi bora ya kutinga ndani ya nafasi saba.

Chelsea iko na ubora wa magoli manne huku Man U ikiwa tu na goli moja hivyo basi kujipata katika miereka ya ubabe iliyo na uhasama wa kutaniana kila mmoja ajikwae.

Mara 18 ambazo Burnley wamekutana na Man U, mashetani hao wekundu wameshinda mara 11, wakashindwa mara mbili na wakatoka sare mara tano.