Michezo

Manchester United kurefusha mkataba wa Pogba ugani Old Trafford

October 19th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamefichua mpango wa kurefusha mkataba wa kiungo Paul Pogba uwanjani Old Trafford kwa mwaka mmoja zaidi hadi 2022.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 27 alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyakua ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo 2018.

Mkataba wake wa sasa na Man-United ulitarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Pogba amepangwa na Man-United katika kikosi cha kwanza kwenye mechi zote tatu za hadi kufikia sasa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ikiwemo ile iliyowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 6-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur uwanjani Old Trafford mnamo Oktoba 4, 2020.

Mnamo Oktoba 9, 2020, Pogba alisema kwamba kubwa zaidi katika matamanio yake ni kuchezea Real Madrid au Barcelona nchini Uhispania kabla ya kustaafu soka.

Pogba alijiunga upya na Man-United kutoka Juventus kwa kima cha Sh12 bilioni mnamo 2016. Jeraha la kifundo cha mguu lilimweka nje ya kampeni za Man-United msimu uliopita wa 2020-21 kwa kipindi kirefu na akawajibishwa mara 22 pekee.