Michezo

Manchester United kuvaana na Real Sociedad nao Arsenal kuonana na Benfica katika hatua ya 32-bora ya Europa League

December 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BAADA ya kushuka ngazi hadi Europa League kufuatia kubanduliwa kwao kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, Manchester United watavaana sasa na Real Sociedad ya Uhispania kwenye hatua ya 32-bora msimu huu.

Mechi hizo za mikondo miwili zinatarajiwa kukutanisha Man-United na aliyekuwa nahodha na kiungo matata wa Manchester City, David Silva aliyeingia katika sajili rasmi ya Sociedad mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal watavaana na miamba wa soka ya Ureno, Benfica huku Tottenham Hotspur ambao kwa sasa wanaongoza jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wakichuana na Wolsberger kutoka Austria.

Leicester City ambao ni wawikilishi wengine wa soka ya Uingereza kwenye kampeni za Europa League msimu huu watacaana na Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech huku viongozi wa Ligi Kuu ya Scotland, Rangers wakitiwa katika zizi moja na Royal Antwerp kutoka Ubelgiji.

Mechi zote za mkondo wa kwanza na pili katika hatua ya 32-bora ya Europa League msimu huu zimeratibiwa kusakatwa mnamo kati ya Februari 18-25, 2021.

Mshindi wa Europa League muhula huu atafuzu kwa kivumbi cha UEFA mnamo 2021-22.

Mabingwa watetezi wa Europa League, Sevilla kutoka Uhispania hatashiriki kivumbi cha msimu huu wa 2020-21 kwa sababu wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA. Kikosi hicho kinachonolewa na kocha Julen Lopetegui kinajivunia kutwaa taji la Europa League mara sita chini ya kipindi cha miaka 14 iliyopita.

Droo ya hatua ya 32-bora ya Europa League:

Wolfsberger na Tottenham

Dynamo Kyiv na Club Brugge

Real Sociedad na Manchester United

Benfica na Arsenal

Red Star Belgrade na AC Milan

Royal Antwerp na Rangers

Slavia Prague na Leicester

RB Salzburg na Villarreal

Braga na AS Roma

Krasnodar na Dinamo Zagreb

Young Boys na Bayer Leverkusen

Molde na Hoffenheim

Granada na Napoli

Maccabi Tel-Aviv na Shakhtar Donetsk

Lille na Ajax

Olympiakos na PSV Eindhoven