Michezo

Manchester United waponda Leeds United na kupaa hadi tatu-bora EPL

December 20th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

SCOTT McTominay aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili chini ya dakika tatu za ufunguzi wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alipowasaidia waajiri wake Manchester United kudhalilisha Leeds United 6-2 mnamo Jumapili ugani Old Trafford.

Kiungo huyo aliwafungulia Man-United karamu ya mabao baada ya sekunde 67 pekee kabla ya kufunga goli la pili sekunde chache baadaye kwa kukamilisha krosi ya Anthony Martial.

Bruno Fernandes na Victor Lindelof walitikisa pia nyavu za Leeds United katika dakika za 20 na 37 mtawalia kabla ya Liam Cooper kurejesha waajiri wake mchezoni kupitia bao la kichwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Daniel James alifungia Man-United bao la nne katika dakika ya 65 kabla ya Fernandes kuongeza goli lake la pili kupitia penalti iliyotokana na tukio la Martial kuchezewa visivyo na Pascal Struijk ndani ya kijisanduku.

Stuart Dallas aliwapachikia Leeds United bao la pili kunako dakika ya 73 kwenye mchuano huo wa kusisimua ulioshuhudia jumla ya makombora 43 yakivurumishwa na wachezaji wa vikosi vyote viwili.

Ushindi kwa Man-United wanaotiwa makali na kocha Ole Gunnar Solskjaer uliwapaisha miamba hao wa soka ya Uingereza hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 26 sawa na Everton waliopepeta Arsenal 2-1 ugani Goodison Park mnamo Disemba 19.

Kwa upande wao, Leeds United walisalia katika nafasi ya 14 kwa pointi 17, saba pekee nje ya mduara ulio na vikosi vilivyopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za muhula huu wa 2020-21.

Hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Leeds United kwa mara ya kwanza ligini baada ya miaka 16, Man-United walikuwa wameshinda mechi moja pekee katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu.

Isitoshe, kikosi hicho kilikuwa kimefunga mabao matatu pekee ugani Old Trafford licha ya kutikisa nyavu za wapinzani angalau mara tatu katika kila mojawapo ya mechi sita ambazo wamesakata ugenini kufikia sasa.

Hadi alipowaongoza Man-United kuponda Leeds United ligini, McTominay ambaye ni raia wa Scotland alikuwa amewafungia waajiri wake magoli sita pekee kutokana na mechi 68 za awali.

Mbali na Cooper na Dallas, wanasoka wengine walioridhisha zaidi kambini mwa Leeds United wanaotiwa makali na kocha Marcelo Bielsa, ni Patrick Bamford na Raphinha Belloli waliopoteza nafasi nyingi za wazi.

Nusura Jack Harrison afanye mambo kuwa 6-3 sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa ila akakosa kulenga shabaha kwenye lango la Man-United lililokuwa chini ya ulinzi wa kipa David De Gea.