Michezo

Manchester United wasuka njama ya kuangamiza Palace

August 24th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United inatarajiwa kuendeleza ukatili wake dhidi ya Crystal Palace itakayozuru uwanjani Old Trafford kwa mechi ya ligi, leo Jumamosi.

United, almaarufu Red Devils, haijapoteza mechi dhidi ya Palace katika mechi 20 zilizopita ligini. Ina ushindi 21, sare tano na kichapo kimoja dhidi ya Palace katika mechi 27 zilizopita katika mashindano yote.

Wachezaji Anthony Martial, Marcus Rashford, Juan Mata na Paul Pogba wanatarajiwa kuongoza juhudi za United kutafuta ushindi baada ya kukabwa 1-1 katika mechi iliyopita dhidi ya Wolves.

Akipata bao leo, Martial atakuwa mchezaji wa nne wa United kufunga katika mechi tatu za kwanza za msimu baada ya Dwight Yorke msimu 1999-2000, Ruud van Nistelrooy (2005-2006) na Wayne Rooney (2011-2012).

Mata amefungia ‘Red Devils’ mabao manne dhidi ya ‘Eagles’, mabao ambayo hakuna mchezaji mwingine wa United katika kikosi cha sasa amewahi kufikisha kwa hivyo mchuano huu unampa fursa nzuri ya kujituma zaidi ili kuimarisha rekodi yake.

Palace, ambayo ilikaba United 0-0 ilipozuru Old Trafford mara ya mwisho Novemba mwaka jana, inaongozwa na Roy Hodgson.

‘Kupoteza hajawahi’

Kocha huyu hajawahi kushinda uwanjani humu akiongoza Blackburn, Fulham, Liverpool, West Bromwich na Palace.

Atatumai kuwatumia wachezaji kama Jeffrey Schlupp, Wilfried Zaha, Christian Benteke na Andros Townsend kumaliza nuksi za kutoshinda United ligini tangu ilipoichabanga 3-0 mwaka 1991. Mara ya mwisho United ilipoteza dhidi ya Palace katika mashindano yoyote ni mwaka 2011 ilipolemewa 2-1 katika soka ya muondoano ya League Cup.

Palace ilifanya vyema ugenini kuliko klabu zote msimu uliopita. Vijana wa Hodgson walizoa alama 29 katika ardhi ya wenyewe kwa hivyo United inafaa kuwa macho.

Tangu ajiunge Palace mwezi Januari 2017 nahodha Luka Milivojevic amefunga penalti 19 katika Ligi Kuu ya Uingereza, nane zaidi ya mchezaji yeyote mwingine.