Michezo

Manchester United wawapa West Brom kibarua cha kusuburi zaidi ushindi wa kwanza EPL

November 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

PENALTI iliyofungwa na Bruno Fernandes baada ya mkwaju wake wa kwanza kupanguliwa na kipa Sam Johnstone ilitosha kuwapa Manchester United ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Novemba 21, 2020 ugani Old Trafford.

Johnstone ambaye ni kipa wa zamani wa Man-United, alifanya kazi ya ziada ya kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Fernandes, Anthony Martial, Edinson Cavani na Marcus Rashford.

Licha ya Johnstone kupangua penalti iliyochanjwa na Fernandes mara ya kwanza, refa aliibatilisha baada ya teknolojia ya VAR kubaini kwamba kipa huyo alikuwa ametoka tayari kwenye mstari wa goli wakati wa kupigwa kwa mkwaju huo.

Fernandes hakukosea tena alipopata fursa ya pili ya kupiga penalti na akakomesha ukame wa dakika 324 ulioshuhudia Man-United bila bao kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafford. Hadi walipofunga dhidi ya West Brom, bao la mwisho la ligi lililojivuniwa na Man-United ugani Old Trafford ni penalti ya Fernandes katika kichapo cha 6-1 walichopokezwa na Tottenham Hotspur mnamo Oktoba 4, 2020.

Kichapo ambacho West Brom walipokezwa kilikuwa kichungu zaidi kwao hasa ikizingatiwa kwamba VAR iliwanyima penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya Fernandes kumchezea visivyo fowadi Conor Gallagher ndani ya kijisanduku.

Baada ya kurejelea mtambo wa VAR, refa David Coote alibatilisha maamuzi yake ya awali ya kuwapa West Brom mkwaju wa penalti, jambo ambalo lililalamikiwa pakubwa na kocha Slaven Bilic.

Matokeo hayo yaliwasaza West Brom ambao walikosa huduma za nahodha Jake Livermore na beki Kieran Gibbs wanaouguza Covid-19, katika ulazima wa kusubiri zaidi kujizolea alama ya kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Baada ya kusajili ushindi mara mbili mfululizo kwenye EPL, Man-United walipaa hadi nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 13 sawa na Everton, Crystal Palace na Wolves.

Ushindi huo wa Man-United ambao waliwaruka Manchester City jedwalini, ulimpa kocha Ole Gunnar Solskjaer kitulizo kikubwa hasa ikizingatiwa presha iliyokuwa ikimkabili kabla ya ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na vijana wake dhidi ya Everton mnamo Novemba 7, 2020.

Kichapo cha 2-0 ambacho Man-City walipokezwa na Tottenham Hotspur katika mechi nyingine ya EPL kiliwasaza masogora wa kocha Pep Guardiola katika nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 12.

Johnstone alihudumu kambini mwa Man-United kwa kipindi cha miaka tisa kabla ya kujiunga na West Brom mnamo 2018.

Man-United kwa sasa wamepiga West Brom katika EPL ugani Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2015 ambapo walisajili ushindi wa 2-0. Mechi mbili za awali kabla ya hiyo ya 2015 zilikamilika kwa sare na ushindi kwa upande wa West Brom.

Mechi dhidi ya West Brom iliwapa Man-United pia ushindi wa kwanza katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu na hivyo kukomesha rekodi mbaya iliyowashuhudia wakikosa kuvuna ushindi katika mechi sita mfululizo (sare tatu na kupoteza tatu) tangu Julai 2019 walipopepeta Bournemouth 5-2.

West Brom kwa sasa wameshindwa kusajili ushindi katika mechi tisa za ufunguzi wa msimu katika EPL kwa mara ya kwanza tangu 1985-86. Kikosi hicho cha kocha Bilic kimeambulia sare mara tatu na kupoteza michuano sita.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuwaalika Basaksehir kutoka Uturuki kwa minajili ya gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 24 kabla ya kuwaendea Southampton ligini mnamo Novemba 29. Kwa upande wao, West Brom wamepangiwa kuwa wenyeji wa Sheffield United mnamo Novemba 29, 2020.