Michezo

Manchester United wazamisha Crystal Palace kusalia unyo kwa unyo na Leicester City ligini

July 17th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United waliendeleza ubabe wao katika juhudi za kuwania nafasi ya kunogesha kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao kwa kuwatandika Crystal Palace 2-0 uwanjani Selhurst Park.

Man-United walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakitawaliwa na presha ya kusajili ushindi baada ya Leicester City ambao ni washindani wao wakuu katika vita vya kutinga ndani ya mduara wa nne-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kuwapepeta Sheffield United 2-0 katika gozi la awali uwanjani King Power.

Ushindi kwa Man-United ambao wanatiwa makali na kocha Ole Gunnar Solskjaer uliwadumisha katika nafasi ya tano kwa alama 62 sawa na Leicester wanaowazidi kwa wingi wa mabao.

Marcus Rashford aliwafungulia Man-United ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya ushirikiano kati yake na kiungo Bruno Fernandes kuchangia bao la pili lililojazwa kimiani na Anthony Martial katika dakika ya 78.

Ufanisi huo wa Man-United uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwao katika jumla ya mechi 19 zilizopita katika mapambano yote.

Kipindi cha kwanza kilikamilika kwa wingi wa hisia kali kutoka kwa wanasoka wa Palace waliohisi kunyimwa penalti baada ya mshambuliaji Wilfried Zaha kukabiliwa visivyo na beki Victor Lindelof ndani ya kijisanduku.

Isitoshe, bao la fowadi Jordan Ayew aliyedhani alikuwa amewasawazishia Palace katika dakika ya 55 lilifutiliwa mbali na refa baada ya kutumia teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alicheka na nyavu za Man-United wakati akiwa ameotea.

Hiyo ilikuwa mechi ya sita kwa kikosi cha Palace kupoteza kwa mfululizo chini ya kocha Roy Hodgson. Pigo kubwa zaidi kwa mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza ni ulazima wa kukosa huduma za beki Patrick van Aanholt katika michuano miwili ya mwisho wa msimu huu baada ya kupata jeraha baya la bega alipokuwa akiwania mpira kutoka kwa Martial.

Man-United walisalia kumsifia kipa David De Gea aliyefanya kazi ya ziada ya kupangua makombora aliyoelekezewa na Luka Milivojevic na Zaha.

 

Straika wa Manchester United Anthony Martial (kati) apiga mpira na kufunga bao ambalo ni la pili mchezoni ‘Mashetani Wekundu’ walipocheza dhidi ya Crystal Palace uwanjani Selhurst Park Julai 16, 2020. Picha/ AFP

Man-United kwa sasa wanasalia katika vita vya kufukuzia nafasi ya kufuzu kwa kipute cha UEFA na iwapo wataambulia nje ya mduara wa nne-bora hatimaye, basi watanogesha kivumbi cha Europa League msimu ujao. Aidha, wanapigiwa upatu wa kuzamisha Chelsea katika nusu-fainali ya Kombe la FA itakayowakutanisha uwanjani Wembley mnamo Julai 18, 2020 na hatimaye kunyanyua ubingwa wa taji hilo kwa mara ya 13 katika historia.

Kwa upande wao, Palace wamepangiwa kuvaana na Wolves mnamo Julai 20 uwanjani Molineux kabla ya kuwaalika Tottenham Hotsour ugani Selhurst kwa mechi ya EPL mwisho msimu huu mnamo Julai 26.

Baada ya kupimana ubabe na Chelsea katika Kombe la FA, Man-United ambao pia wanafukuzia ufalme wa Europa League msimu huu, wamepangiwa kukwaruzana na West Ham United uwanjani Old Trafford kabla ya kuwaendea Leicester City katika michuano miwili ijayo ya EPL.

MATOKEO YA EPL (Julai 16, 2020):

Everton 1-1 Aston Villa

Leicester 2-0 Sheffield United

Crystal Palace 0-2 Man-United

Southampton 1-1 Brighton