Michezo

Manchester United yamezea mate Eriksen wa Spurs, Arsenal ikitaka Upamecano wa RB

August 8th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United wamefanya mazungumzo kwa lengo la kumsajili Christian Eriksen wa Tottenham, lakini kiungo huyo anawania kuhamia Uhispania.

Mabingwa hao wa ligi kuu mara 20 wamekuwa wakivutiwa na staa huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa muda mrefu.

Raia huyo wa Denmark mwenye thamani ya Sh6.7 bilioni tayari anakodolewa macho na klabu za Real Madrid, Atletico madrid na Juventus, lakini macho yake yanalenga La Liga.

Ripoti zimesema ingawa roho yake haitaki kuendelea kucheza kwenye ligi kuu ya Uingereza (EPL), huenda akalazimika kujiunga na Manchester United baada ya maafikiano.

Uvumi kuhusu aliyekuwa staa wa Spurs Fernando Lolorente kukaribia kujiunga na Manchester United umekuwa wa kushtua wengi, na pia kuna uwezekanao wa Paul Dybala kutua ili achukue nafasi ya Romelu Lukaku anayejiandaa kuyoyomea Juventus.

Arsenal

Kwingineko, Arsenal wameambiwa lazima walipe Sh10.5 bilioni kumtwaa Dayon Upamecano kutoka RB Leipzig kabla ya dirisha la usajili kufungwa leo Alhamisi usiku, ingawa Leipzig imesisitiza kuwa haitamuachilia.

Baada ya kukamilisha usajili wa Nicolas Pepe kutoka Lille kwa kitita cha Sh10.8 bilioni, Arsenal inajiandaa kumnasa Upamecano, Mfaransa anayechezea timu ya taifa ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21.

Ripoti kutoka nchini Ujerumani zimedai kwamba RB ilikataa ofa ya 8.2 bilioni kutoka kwa Arsenal, mwishoni mwa wiki.

Upamecano aliyoyomea nchini Ujerumani mnamo 2015 akiwa mdogo baada ya kukataa kujiunga na Manchester United.

Kadhalika Arsenal imeonyesha nia ya kumtaka Daniele Rugani wa Juventus ambaye thamani yake imesemekana kuwa Sh7.5 bilioni.