Michezo

Manchester United yaotea kupokonya Aston Villa mkali wao Watkins

May 18th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

MANCHESTER United inalenga kuwasilisha ofa nzuri ili kumtwaa mfungaji bora wa Aston Villa, Ollie Watkins.

Watkins amekuwa wembe shoka la Aston Villa kufyeka wapinzani akiwasaidia kufuzu Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hata kabla mechi yao kutamatisha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Villa tayari imejihakikishia kumaliza nambari nne ligini baada ya washindani wao wakuu Tottenham Hotspur kupigwa katikati mwa wiki.

Villa ina alama 68 huku Tottenham ikiwa na 63 ambazo hazitoshi kurukia namba nne hata iwapo Villa itashindwa siku ya mwisho ya ligi Jumapili.

Watkins, 28, anaonekana kama anayetosha mboga safu ya mashambulizi ya Man-United kuwinda magoli msimu ujao akisaidiana na mvamizi Rasmus Hojlund.

Msimu huu raia huyo wa Uingereza ametinga magoli 27 kwenye mashindano yote ambayo Aston Villa imeshiriki.

Kibarua kwa Man-United, hata hivyo, ni kushawishi Villa waachilie mchezaji ambaye alitia saini mkataba wa miaka mitano mwaka 2023.

Ili kupata pesa za kumnunua Watkins – na wakati huo huo kupunguza gharama yao ya mishahara – Red Devils watauza wachezaji wake wengi hususan wanaokula mihela mikubwa kikosini kama vile Raphael Varane, Casemiro, Christian Eriksen na Antony Martial.

Imekusanywa na Cecil Odongo