Michezo

Manchester United yasaka kizibo cha De Gea anayemezewa PSG

May 24th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United wanajiandaa kutafuta huduma za kipa wa AC Milan, Gianluigi Donnarumma baada ya madai kwamba David de Gea amekataa ofa ya mwisho ya kuongeza kandarasi kutoka kwa waajiri wake.

Ikiwa Milan itakosa kufuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya, huenda mlango wa Donnarumma kuhama ukafunguliwa.

Vita vya kufuzu kushiriki michuano ya Klabu Bingwa bado ni vikali kwenye Ligi Kuu ya Italia, huku alama tatu pekee zikitofautisha nambari tatu Atalanta na AS Roma inayoshikilia nafasi ya sita.

Milan kwa sasa inashikilia nafasi ya tano kwenye jedwali na ikiwa itakosa kumaliza ligi ndani ya mduara wa klabu nne-bora, basi Donnarumma huenda akawa mbioni kuyoyomea kwingineko, tovuti ya Calciomercato nchini Italia inasema.

Klabu ya Milan ina jumla ya alama 65, pointi moja nyuma ya majirani na mahasimu wa tangu jadi Inter.

Inasemekana Milan isipoingia Klabu Bingwa, ajenti wa kipa huyu, Mino Raiola, atatafuta njia ya mteja wake kuondoka. Donnarumma anatambuliwa kama mmoja wa makipa wazuri nchini Italia na amekosa mechi mbili pekee za Milan ligini tangu aisakatie mechi ya kwanza mwaka 2015.

Baada ya Milan kubwaga Frosinone 2-0 juma lililopita, mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 20 alipuuza maswali yaliyoulizwa kuhusu uwepo wake katika klabu hiyo.

“Sipendi kuzungumzia suala hilo,” alinukuliwa na gazeti la Corriere della Sera nchini Italia.

Donnarumma ana kandarasi na Milan hadi mwaka 2024, ingawa mshahara wake, unaoaminika kuwa Sh676.3 milioni kila mwaka, huenda ukawa mzigo sana kulipia klabu hiyo isipopata mapato zaidi yanayoongezeka kwa kucheza katika Klabu Bingwa.

Tovuti ya Calciomercato inadai kwamba ombi la kati ya Sh6.7 bilioni na Sh7.8 bilioni huenda likatosha kushawishi Milan kuruhusu kipa huyo chipukizi kuondoka Italia.

De Gea akataa ofa ya mwisho

Hamu ya United kusajili Donnarumma inatokana na kuwa De Gea alikataa ofa ya mwisho.

Inasemekana kwamba Mhispania huyo anataka mshahara wake uongezwe kutoka Sh25.5 milioni kwa wiki hadi Sh44.7 milioni, kiasi ambacho Paris-Saint Germain iko tayari kumpa kipa huyo mwenye umri wa miaka 28.

De Gea anakaribia kuingia miezi 12 ya mwisho kwenye kandarasi yake na United italazimika kufanya uamuzi wa haraka ama impoteze mwaka ujao bila ya kupata kitu.