Michezo

Manchester United yazidi kukaa ngumu kuhusu Pogba

August 15th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United haitakubali ofa yoyote kwa mchezaji wake Paul Pogba kabla ya kipindi cha uhamisho cha Bara Ulaya kufungwa mapema mwezi ujao, tetesi zinasema.

Pogba, 26, alikiri kuwa bado hana uhakika muda atakaoendelea kuwa uwanjani Old Trafford baada ya United kuaibisha Chelsea 4-0 Jumapili katika mechi ambayo alimega pasi zilizozalisha mabao mawili ya mwisho.

Huku vipindi vya uhamisho nchini Uhispania na Italia vikikamilika Septemba 2, kuna fununu kuwa klabu za Real Madrid na Juventus zitazidi kujaribu bahati yao kupata Pogba.

Hata hivyo, ripoti zinasema kuwa United ina sababu kadhaa zitakazoifanya imkwamilie Pogba.

Kwanza ni kuwa kocha Ole Gunnar Solskjaer anaona Pogba kuwa sehemu muhimu katika mipango yake ya msimu huu. Baada ya kuvutiwa na mtazamo na mchezo wa kiungo huyo kwa kumsoma kwa kina, anaamini kuwa Mfaransa huyo atamakinikia kazi iliyoko mbele yake.

Pili, kufuatia kufungwa kwa kipindi cha uhamisho nchini Uingereza mnamo Agosti 9, United haitapata kizibo chake. Baada ya kukosa kuimarisha safu ya kati katika kipindi cha uhamisho kilichopita, United si imara sana katika idara hiyo.

United haikuwa tayari kupoteza Pogba katika kipindi hicho cha uhamisho, ingawa haingesita kuuza Mfaransa huyu anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji ghali katika klabu hii ya Sh11 bilioni kama klabu yoyote ingewasilisha ofa isiyopungua Sh19.9 bilioni.

Hakuna klabu hata moja ilikaribia bei hiyo, hata hivyo, na hali haitarajiwi kuwa tofauti wiki chache zijazo, na hata ofa kama hiyo ikitokea, United inasemekana itapuuza wazo la kuachilia Pogba.

Ofa ya Real ya Sh3.5 bilioni pamoja na mshambuliaji wa Colombia James Rodriguez ilikataliwa na United wiki mbili zilizopita.

Mpango huo wa Real ulifanya United kuamini zaidi kuwa miamba hao wa Uhispania hawana fedha za kutangaza ofa inayofaa baada ya kutumia zaidi ya Sh33.6 bilioni kusajili wachezaji wapya akiwemo Eden Hazard kutoka Chelsea.

Ushawishi

Msimamo wa United hautarajiwi kuzika kabisa uvumi wa muda mrefu kuwa Pogba ataondoka Old Trafford.

Cristiano Ronaldo, ambaye alikataa kuwa haelekei Real mwaka 2008, alishawishiwa na kocha wa zamani Sir Alex Ferguson kuchezea United kwa msimu mmoja zaidi kabla ya kuhama ikiwa alihisi alihitaji kufanya hivyo.

Haijabainika kama Solskjaer amefanya mpango kama huo na Pogba. Pogba atasalia na miaka miwili katika kandarasi yake baada ya msimu huu, ingawa bado bei yake itakuwa juu na pia waajiri wapya watahitaji kumlipa mshahara wake wa Sh36.1 milioni kila wiki.

Pia, haijulikani kama United itaanzisha mazungumzo ya kutafuta kumuongeza kandarasi msimu ujao.

Hata hivyo, Mfaransa huyu amekuwa akipigania kuondoka Old Trafford kwa misimu miwili sasa. Aliomba aruhusiwe ajiunge na Barcelona, lakini ombi lilikataliwa.