Makala

Manda-Maweni: Kijiji cha maisha magumu kwa mtu kifyefye 1GB

February 1st, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MANDA-Maweni ni kijiji cha Lamu kilichoanzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Kijiji hicho hupatikana eneobunge la Lamu Magharibi.

Ili kukifikia kijiji hicho kilichoko mashambani, mja hulazimika kutumia mbinu mbalimbali za usafiri, ikiwemo ule wa boti na mashua, ambapo huvuka maili kadhaa ndani ya Bahari Hindi kabla ya kufika ng’ambo ya pili.

Baadaye msafiri huunganisha safari hiyo kwa kutumia pikipiki, ambapo barabara yenyewe inayotumiwa huwa ni ya vumbi na mashimo kabla ya kufikia kijiji cha Manda-Maweni.

Ni kisiwa hiki ambacho pia magari hakuna isipokuwa baiskeli, pikipiki na punda pekee wanaohudumia uchukuzi wa eneo hilo.

Unapoingia kijiji cha Manda-Maweni, utakaribishwa na sanamu ya binadamu aliyebeba matofali na anayeonekana bayana kustahimili uzito wa mzigo huo.

Sanamu ya binadamu aliyebeba mawe ya kujengea katika kijiji cha Manda-Maweni, Lamu Magharibi. Maisha huko ni magumu hasa kwa mtu kifyefye 1GB. PICHA | KALUME KAZUNGU

Sanamu hiyo inadhihirisha wazi taswira kamili ya kijiji cha Manda-Maweni kwamba maisha hapa si rahisi unavyodhania.

Yaani kwa wakazi wa kijiji hiki wanaamini tu jambo moja, nalo ni “kula kwa jasho lako.”

Ni Manda-Maweni ambapo maisha huwawia magumu watu vifyefye au kwa lugha rahisi 1GB.

Kitega uchumi cha pekee kwenye kijiji cha Manda-Maweni ni uchimbaji na uchongaji wa matofali, kuvunja changarawe na kokoto za kujengea nyumba.

Baadaye mawe hayo huhitajika kubebwa hadi kwenye ufukwe wa kijiji hicho, ambapo ndiyo bandari halisi ya vifaa hivyo kubebwa na kusafirishwa kuvukishwa maeneo mengine ya Lamu kuendeleza ujenzi mbalimbali.

Ni kutokana na hilo ambapo lazima mja hapa kujikakamua vilivyo, ambapo watu mapandikizi na wenye bidi ndio wanaojikuta maisha yakiwaendea nywe.

Benson Irungu, mmoja wa wachimba mawe kwenye migodi ya Manda-Maweni, anasema ili kufaulu maishani, wakazi wa kijiji hicho wametambua umuhimu wa kuamka mapema kwenda kwenye machimbo ya mawe kutekeleza kazi zao.

Bw Irungu anasema kwa wengi wanaotekeleza kazi hiyo, kurudi nyumbani huwa ni jioni ya kuchelewa.

“Hatuna kazi nyingine ya maana hapa Manda-Maweni isipokuwa kuchimba mawe. Ndio sababu utapata kila mahali pakiwa pamesheheni machimbo. Hapa wavivu hawawezi kustahimili mawimbi ya maisha magumu. Lazima mja ujitume, uchanike mpinini kila siku ndipo uishi hapa,” akasema Bw Irungu.

Justus Mwaniki Mwaniki, ambaye hutekeleza kazi ya kusafirisha matofali kwa punda kutoka machimboni hadi bandarini anaamini kuwa mtu mwenye uwezo wa kuishi kijiji cha Manda-Maweni hawezi kushinda na maisha mahali popote atakapojikuta nchini Kenya.

“Maisha magumu tumeyazoea hapa. Usafiri ni tabu. Uhaba wa maji uko hapa. Kazi ni za sulubu. Vituo vya afya ni balaa nakadhalika. Kama waweza kuishi Manda-Maweni wewe ni shujaa unayeweza kuishi sehemu yoyote ile nchini, iwe ni ngumu ama ya raha mustarehe,” akasema Bw Mwaniki.

Bi Lilian Okoth, ambaye kazi yake ni kuvunja na kubeba changarawe na kokoto za kujengea kijijini Manda-Maweni anasema kazi yoyote ni kazi kwa wakazi wa kijiji hicho cha mashambani.

Bi Okoth anasema maisha magumu wanayoyaishi Manda-Maweni yamewafunza kutobagua kazi ilmradi mja apati mtaji wa kujikimu maishani.

“Kuna wengine huwa wanasema kuna kazi za jinsia ya kike na ile ya kiume. Hapa Manda-Maweni hilo halipo. Iwe ni mwanamume au mwanamke utafanya kazi yoyote hapa, iwe ni kuingia machimboni kuvunja na kuchonga mawe au kuzoa kokoto ndipo uishi hapa,” akasema Bi Okoth.

Kijiji cha Manda-Maweni kina zaidi ya wakazi 2000, wengi wakiwa ni wale wa jamii za Wajaluo, Wakisii, na Wagiriama waliohamia eneo hilo kutoka maeneno mengine ya nchi miaka ya 1980 ili kuendeleza kazi hiyo ya kuchimba mawe.

Mkazi wa Manda-Maweni akiwa amebeba matofali kijijini humo. PICHA | KALUME KAZUNGU