Makala

MANDERA: Serikali lawamani kwa utovu wa usalama

October 15th, 2018 2 min read

Na MANASE OTSIALO

VIONGOZI katika Kaunti ya Mandera wamelaumu serikali kwa ukosefu wa usalama katika eneo hilo. Viongozi hao walisema hayo kufuatia shambulizi lililotekelezwa na magaidi wa Al Shabaab katika Shule ya Wavulana ya Arabia na kusababisha vifo vya walimu wawili wiki moja iliyopita.

Mbunge wa Mandera Mashariki Bw Omar Maalim na aliyekuwa naibu gavana wamehusisha ongezeko la mashambulizi eneo hilo na uhaba wa maafisa wa usalama.

“Arabia ni Kaunti Ndogo inayotambuliwa Mandera lakini tangu kubuniwa kwake hatuna afisi zinazopaswa kuwepo katika kiwango cha wilaya,” alisema Bw Maalim

Bw Maalim alisema Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amepuuza Arabia tangu ilipobuniwa kutoka Mandera Mashariki 2017.

Arabia na Kotulo zilitangazwa kuwa Kaunti Ndogo Juni 21, 2017 kupitia toleo la gazeti rasmi la serikali lakini ni Kotulo pekee iliyo na Naibu Kamishna.

“Kaunti Ndogo huwa na afisi za Naibu Kamishna na afisi zote za usalama zinazohitajika na hilo likifanyika ukosefu wa usalama Arabia utakabiliwa,” alisema. Diwani wa Arabia Bw Abdiaziz Dakat, alihusisha ukosefu wa usalama na uhaba wa maafisa.

“Naibu kamishna atakapotumwa hapa itamaanisha afisi nyingine zote zitakuwemo na Arabia itakuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na shida zake badala ya kutegemea Mandera Mashariki,” alisema.

Kituo cha kipekee cha polisi kwenye mpaka wa Kenya na Somalia kimeshambuliwa mara mbili na magaidi wa Al Shabaab kutoka Somalia.

“Tutakuwa na afisa wa cheo cha juu cha polisi na vitengo vya kutosha vya usalama vinavyohudumu eneo hili,” alisema Bw Dakat.

Diwani huyo alisema kuchelewa kutuma maafisa wa serikali eneo hilo kumecheleweshea wakazi huduma muhimu.

“Wale wanaotaka huduma za serikali kama vyeti vya kuzaliwa hawawezi kuvipata Mandera Mashariki kwa sababu inajulikana kwamba Arabia ni wilaya,” alisema

Viongozi hao walikubaliana kuwa Arabia ikiwa na afisi zinazofanya kazi, usalama katika barabara ya Mandera-Omar Jillow- Arabia utaimarika. Serikali ya kitaifa ilifunga barabara hiyo 2015 baada ya magaidi wa Al Shabaab kushambulia basi na kuua watu 28.