Mane afikisha mabao 100 akivalia jezi za Liverpool

Mane afikisha mabao 100 akivalia jezi za Liverpool

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL waliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi kufikia sasa msimu huu baada ya fowadi Sadio Mane kupachika wavuni bao lake la 100 akivalia jezi za klabu hiyo katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Crystal Palace.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walipata nafasi nyingi za kuzamisha chombo cha Palace waliosalia thabiti katika takriban kila idara. Ilikuwa hadi dakika ya 43 ambapo Mane alifungua ukurasa wa mabao kabla ya magoli mengine kufumwa wavuni na Mohamed Salah na Naby Keita.

Diogo Jota, Thiago Alcantara na Jordan Henderson pia walipoteza nafasi kadhaa za kutikisa nyavu za Palace waliodumishwa mchezoni katika kipindi cha kwanza na kipa Vicente Guaita.

Palace wanaonolewa na kocha Patrick Vieira, walianza vizuri mchuano huo kwa kugonga mhimili wa goli la Liverpool mara mbili. Masogora wa Liverpool walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo siku tatu baada ya kuwacharaza AC Milan 3-2 kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ushindi wa Liverpool uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali la EPL baada ya kushinda mechi nne kati ya tano za ufunguzi wa msimu huu. Palace kwa upande wao kwa sasa wanakamata nafasi ya 14 kwa pointi tano.

Mane alikuwa miongoni mwa wanasoka sita waliowajibikia Liverpool baada ya kuachwa nje katika mechi ya awali dhidi ya AC Milan.Akiwa mfungaji wa mabao mawili ya Liverpool dhidi ya Palace katika siku ya mwisho ya kampeni za EPL mnamo 2020-21, goli la Mane mnamo Jumamosi lilimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga mara tisa mfululizo dhidi ya mpinzani mmoja.

Nyota huyo raia wa Senegal sasa anajivunia jumla ya mabao 13 dhidi ya Palace katika EPL – idadi kubwa zaidi ya magoli ambayo kikosi hicho kimewahi kufungwa na mchezaji mmoja.

Hiyo ilikuwa njia mwafaka zaidi kwa Mane kufikisha mabao 100 akichezea Liverpool katika mapambano yote.Fowadi Wilfried Zaha aliyekuwa akichezea Palace mchuano wake wa 250 katika EPL ndiye aliyeridhisha zaidi dhidi ya Liverpool.

Hata hivyo, alitatizika sana kumzidi ujanja Fabinho na beki Ibrahima Konate aliyewajibishwa na Liverpool kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe kwa Sh4.8 bilioni kutoka RB Leipzig ya Ujerumani mwishoni mwa msimu uliopita.

  • Tags

You can share this post!

Tusker FC yaanza kunusia Sh60 milioni Klabu Bingwa Afrika...

Watford warefusha mkia wa Norwich City kwenye jedwali la EPL