Michezo

Mane aongoza Liverpool kupepeta Chelsea ugani Stamford Bridge

September 21st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walitangaza mapema azma yao ya kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kuwapepeta Chelsea 2-0 uwanjani Stamford Bridge mnamo Septemba 20, 2020.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walitamalaki mchezo kuanzia dakika ya kwanza na wakamiliki asilimia kubwa ya mpira baada ya Chelsea kusalia wachezaji 10 uwanjani beki Andrea Christensen alipoonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo mvamizi Sadio Mane mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ingawa refa Paul Tierney alikuwa awali amemlisha Christensen kadi ya manjano kwa kosa hilo, maamuzi yake yalibalitilishwa na teknolojia ya VAR.

Mane alishirikiana vizuri na Firmino kufunga bao la kwanza katika dakika ya 50 kabla ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kipa Kepa Arrizabalaga dakika nne baadaye na kuwapa Liverpool goli la pili.

Masaibu ya Chelsea katika mchuano huo yaliendelezwa na kiungo Jorginho ambaye alipoteza penalti iliyotokana na tukio la sajili mpya wa Liverpool, Thiago Alcantara kumchezea visivyo sajili mpya wa Chelsea, Timo Werner katika dakika ya 72. Mkwaju wa Jorginho ambaye hakuwa amepoteza penalti 16 zilizopita za Chelsea, ulipanguliwa kirahisi na kipa Alisson Becker.

Masihara ya Kepa ambaye pia alisuasua katika mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Brighton uwanjani Amex huenda sasa yakamponza kabisa kambini mwa Chelsea baada ya kocha Frank Lampard kufichua mpango wa kuja kwa kipa wa Rennes Edouard Mendy kwa kima cha Sh2.8 bilioni.

Kepa ambaye ni kipa ghali zaidi duniani, huenda sasa akakubali kupungizwa mshahara na kuyoyomea Atletico Madrid au Sevilla ama ahiari kusalia ugani Stamford Bridge bila ya kuunga kikosi cha kwanza.

Chelsea walijibwaga ugani wakitawaliwa na motisha ya kuwapokeza Brighton kichapo cha 3-1 katika mechi ya awali huku Liverpool wakisajili ushindi wa 4-3 baada ya kutolewa jasho na limbukeni Leeds United ugani Anfield.

Yalikuwa matarajio ya Lampard kulipiza kisasi dhidi ya Liverpool waliozamisha chombo chao katika michuano ya mikondo miwili msimu uliopita kwa 2-1 ugani Stamford Bridge kisha 5-3 waliporudiana uwanjani Anfield.

Hata hivyo, Chelsea waliyumba na huenda walikosa uthabiti kwa kukosa huduma za wanasoka matata wakiwemo Christian Pulisic, Thiago Silva, Ben Chilwell na Hakim Ziyech wanaoguza majeraha.

Ushindi wa Chelsea dhidi ya Brighton uliwavunia alama 2,000 katika EPL baada ya kusakata jumla ya mechi 1,077. Wanakuwa klabu ya tatu kufikia ufanisi huo tangu 1992 baada ya Manchester United (2,234) na Arsenal (2,014).

Chelsea kwa sasa wanatazamiwa kujinyanyua dhidi ya West Bromwich Albion, Crystal Palace na Southampton katika mechi tatu zijazo.

Tangu watawazwe mabingwa wa EPL mnamo Juni na kukomesha ukame wa miaka 30 ya taji hilo kabatini mwao, Liverpool wamefungwa jumla ya mabao 15 kwenye mechi nane zilzopita za EPL. Hiyo ni idadi ya mabao ambao miamba hao walifungwa katika jumla ya mechi 23 za awali.

Baada ya kumsajili kiungo Alcantara kutoka Bayern Munich kwa kima chs Sh2.8 bilioni, Liverpool walimsajili pia fowadi Diogo Jota kutoka Wolves kwa mkabata wa miaka mitano utakaorasimishwa kwa Sh5.7 bilioni.

Kusajiliwa kwa Jota, 23, kunatazamiwa kumfanya ajaze pengo litakaloachwa na Divock Origi anayehusishwa pakubwa na Manchester City.