Michezo

Mane kushinda UEFA kwaipa Senegal motisha kufukuzia taji la Afcon

June 2nd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAPINZANI wa Kenya katika mechi za makundi za Kombe la Afrika, Senegal wamepata motisha ya kusema watafukuzia taji nchini Misri baada ya mvamizi wao Sadio Mane kuongoza Liverpool kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya siku ya Jumamosi.

Mane alikuwa katika kikosi cha Liverpool kilichodhalilisha Tottenham Hotspur 2-0 na kujishindia taji lao la sita la mashindano hayo makubwa barani Ulaya kupitia mabao ya Mmisri Mohamed Salah na Mbelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi.

Baada ya ushindi huo, shujaa wa zamani wa Liverpool na Senegal, El Hadji Diouf alinukuliwa na vyombo vya habari akimkumbusha Mane kwamba raia wa nchi hiyo wanatarajia makubwa kutoka kwake katika AFCON.

Aidha, Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Matar Ba alieleza wanahabari nchini humo kwamba anatarajia Mane kuendeleza makali hayo katika mashindano ya Afrika yatakayoanza Juni 21 na kumalizika Julai 19 nchini Misri.

“Kuona Sadio akishinda Klabu Bingwa kunatupa hakikisho na kuongeza matumaini yetu. Najua anafurahia ushindi na Liverpool, lakini tunajua pia anawazia AFCON. Azma yetu ni kushinda Kombe la Afrika.”

Senegal itaanza mechi za Kundi C dhidi ya Tanzania hapo Juni 23 siku ambayo pia Kenya itkabiliana na Algeria. Kenya ya kocha Sebastien Migne inafanyia mazoezi yake nchini Ufaransa ambako mastaa wake wakiwemo Victor Wanyama na Michael Olunga wanatarajiwa kambini juma hili.

Habari kutoka Tanzania zilisema Jumamosi kwamba Taifa Stars imeimarisha mazoezi chini ya Mnigeria Emmanuel Amuneke jijini Dar es Salaam.