Michezo

Mane, Salah watiliwa seng'enge wasihame

March 26th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

LIVERPOOL wamepanga kushawishi mshambuliaji Sadio Mane, kipa Alisson Becker na fowadi Mohamed Salah kurefusha mikataba yao uwanjani Anfield.

Watatu hao ambao wamekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha kocha Jurgen Klopp wanahemewa pakubwa na klabu maarufu barani Ulaya.

Huku Mholanzi Van Dijk akiwaniwa na Juventus ya Italia, Mane anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Real Madrid ambao pia wanakeshea maarifa ya Alisson kwa kima cha Sh9 bilioni.

Matarajio ya miamba hao wa Uhispania chini ya kocha Zinedine Zidane, ni kutafuta kizibo kamili cha kipa Thibaut Courtois anayehusishwa na Olympique Lyon ya Ufaransa.

Juventus wamefichua azma ya kufungulia zaidi mifereji yao ya fedha mwishoni mwa msimu huu na kuweka mezani kima cha Sh21 bilioni ili kumshawishi Van Dijk kutua jijini Turin, Italia.

Kufaulu kwao kutamfanya difenda huyo wa zamani wa Southampton kuwa beki ghali zaidi duniani kwa mara ya pili.

Chini ya unahodha wa Van Dijk, timu ya taifa ya Uholanzi iliibuka ya pili katika mashindano ya Uefa Nations League yaliyotawaliwa na Ureno mwaka jana.

Mafanikio yake ndani ya kikosi cha Liverpool na timu ya taifa ni kati ya mambo yaliyomfanya kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Lionel Messi wa Barcelona na Argentina kwenye tuzo za Ballon d’Or mwaka 2019.

Ballon d’Or ni tuzo ya haiba kubwa zaidi ambayo hutolewa kwa Mwanasoka Bora zaidi duniani kila mwaka.

Real wako radhi kujinasia saini ya Mane kwa Sh19 bilioni mwishoni mwa msimu huu na sogora wa zamani wa Liverpool, Momo Sissoko amesisitiza kwamba itakuwa vigumu kwa Klopp kuzuia uhamisho huo.

Mane ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Senegal, anajivunia kuwafungia Liverpool jumla ya mabao 14 hadi kufikia sasa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

“Salah na Mane ambao ni kati ya wachezaji 10 wa haiba kubwa zaidi duniani, wanawaniwa na Real. Sioni chochote kitakachowadumisha nyota hao ugani Anfield baada ya kushindia Liverpool ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana kisha taji la EPL muhula huu,” akatanguliza Sissoko.

Kufikia sasa, Liverpool wanajivunia pengo la alama 25 zaidi kileleni mwa jedwali la EPL na dalili zote zinaashiria kuwa watatawazwa mabingwa wa kipute hicho.

“Ninaona Mane akiwa mchezaji wa Real msimu ujao. Atakuwa kizibo kamili cha Gareth Bale ambaye anahusishwa na uwezekano wa kuyoyomea China au kurejea Uingereza kuchezea Man-United,” akasema Sissoko kwa kusisitiza kwamba Zidane atashawishika zaidi kumsajili Mane badala ya Salah.