Maneno suka, shuka na zuka yana baidi kubwa kimaana

Maneno suka, shuka na zuka yana baidi kubwa kimaana

NA ENOCK NYARIKI

NENO linaweza kuwa sahihi kisarufi ila linapokosewa katika matamshi, hupotosha maana iliyokusudiwa. Yapo maneno mengine ambayo baadhi ya watu hushindwa kenyekenye kuyatamka kwa sababu ala zao za kutamkia sauti fulani huwa na kasoro fulani.

Kwa mfano, kuna wale ambao hawawezi kabisa kulitamka neno mazishi. Badala yake hulitamka neno hilo kama *mashishi. Anayekosea matamshi ya neno hili huenda akaeleweka kwa urahisi kwa sababu hapana neno jingine la Kiswahili lenye maendelezo kama hayo.

Hata hivyo, lugha ya Kiswahili inapokuwa na neno sawa na lile lililokosewa kimatamshi, hali hiyo hutatiza mazungumzo kwa sababu huenda ikamchukua muda fulani mzungumziwa kuelewa ujumbe unaowasilishwa.

Mathalan, baadhi ya watu wanapotaka kueleza kuwa mtu fulani ameenda kutengenezwa nywele, hutumia neno shuka katika kauli, “Wasichana wameenda *kushukwa!’’ Baadhi ya vitate – neno shuka likiwa miongoni mwavyo – vinapokosewa katika mazungumzo, huzua maana tofauti kabisa na ile iliyokusudiwa.

Kitendo cha kupitisha nywele kwa kupishanapishana ili kuwa na mfumo fulani unaovutia ni kusuka bali si kushuka. Kinyume cha kusuka ni kufumua bali si ‘kubomoa’ jinsi baadhi ya watu hasa wale wa jinsia ya kike hupenda kusema. Kubomoa ni kuharibu kilichojengwa na kusimama wima kama vile ukuta.

Maana nyingine ya neno hilo ni kuharibu mpango au utaratibu fulani. Neno shuka (kitenzi) lina maana mbili. Kwanza ni kutoka juu ya kitu kwa mfano mti au mlima na kuenda chini.

Pili, hutumiwa kibiashara kwa maana ya kupungua kwa thamani ya kitu. Maana nyingine za neno hilo hutegemea miktadha ya matumizi. Kwa mfano, kushuka moyo ni kutokuwa na furaha.

Kitawe

Neno suka ambalo tumeeleza kuwa lina maana ya kutengeneza nywele kwa mfumo unaovutia pia lina maana ya kukitingisha kitu kwa kukipeleka huku na huku kwa mfano chupa yenye kitu kiowevu.

Kitendo cha mnyama, kwa mfano mbwa, kupeleka mkia huku na huku pia ni kusuka. Neno jingine ambalo ni kitate pamoja na suka na shuka ni zuka. Kuzuka ni kutokea ghafla kwa jambo fulani au kutokea kwa jambo ambalo halijawahi kuwepo.

Ni muhimu kutaja kuwa maneno suka na zuka hayatumiwi sana katika mazungumzo yamkini kutokana na sababu mbalimbali. Mojawapo ya sababu hizo ni kuwa ni maneno ambayo matamshi yake huwatatiza baadhi ya wazungumzaji.

Ni rahisi kwa watu hao kutamka neno shuka badala ya suka na zuka. Aidha, maana za maneno yenyewe zimefichika. Kwa hivyo, neno shuka huishia kutumiwa kwa maana finyu ya suka na zuka. Hata hivyo, ni muhimu sana kuyatofautisha maneno hayo matatu ili kurahisisha mawasiliano.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Heri wakubali, kumng’oa Ruto ni kibarua...

Serikali yaanza operesheni ya kuzima ujangili Kapedo