Habari za Kitaifa

Maneno ya mwisho aliyosema Hakimu Kivuti kabla ya kukata roho


IMEFICHULIWA kuwa Hakimu Mwandamizi Monica Kivuti ambaye alifariki baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi kortini alikuwa na wasiwasi kuhusu bintiye wa miezi 18, Elianna Wanjiru, alipokuwa akipigania maisha yake katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Hii ni kulingana na mumewe, Mutimu Kang’ata.

Hakimu huyo aliaga dunia Jumamosi iliyopita kutokana na majeraha ya risasi aliyopata baada ya kushambuliwa na afisa wa polisi.

“Nakumbuka nilipofika kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Metropolitan huko Buruburu. Ulikuwa na maumivu makali lakini uliponiona ulitulia, ukanitazama na kuniuliza: ‘Elianna yukoje?’ Nikakujibu Elianna ni mzima na nimemuacha akilala. Hapo ndipo ulipofunga macho na hukuongea tena. Kwa sasa naelewa kuwa ulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya mwanako mdogo,”

“Hata hivyo, nakuhakikishia kuwa kwa neema ya Mungu nitamlea Elianna. Kwa hivyo huna haja ya kuwa na wasiwasi kumhusu,” Bw Kang’ata alisema wakati wa mazishi wa mkewe katika Kijiji cha Mamba katika Kaunti ya Machakos, Jumamosi.

Mbali na Mtoto Elianna, Bi Kivuti pia aliacha mabinti wengine wawili, Josephine Wanjiru na Michelle Menyi.

Bw Kang’ata alieleza kuwa alikuwa mbioni kutimiza ndoto ya Bi Kivuti ya kutunza familia hiyo katika ardhi waliyonunua miezi minne iliyopita.

Waombolezaji waliitaka  Serikali kufanya mabadiliko kuimarisha mazingira ya kazi ya maafisa wa mahakama.

Kiongozi wa Wiper Bw Musyoka alikashifu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya majaji na mahakimu.

Bw Musyoka ni miongoni mwa waombolezaji waliosema kuwa kifo cha Bi Kivuti kingezuiwa iwapo hakuwa akifanya kazi akiwa kwenye hema.

Alihusisha kifo hicho na ukatili wa polisi ambao alisema umekumba nchi.

“Chini ya katiba ya 2010 tulitarajia mahakama kufanya kazi katika miundomsingi bora. Pia tulitarajia kwamba mahakama itafadhiliwa vyema” Bw Musyoka alisema wakati wa mazishi ya Kivuti katika kijiji cha Mamba katika Kaunti ya Machakos.

Waombolezaji walilaani kupigwa risasi kwa Bi Kivuti na afisa wa polisi Samson Kipchirchir Kipruto, huku wakimsifu hakimu huyo kama mtaalam, mshauri, mama na mke aliyekuwa na upendo.

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alitoa wito kwa Wakenya kuacha kuwaua maafisa wa mahakama..

“Sisi sote tunaofanya kazi katika mahakama ni watu. Tunajua kwamba tutakufa. Niliuliza Jumanne na nitauliza tena: Je, watu wataacha kutuua? Acheni kutuua,” alisema.