Mang’u Youth FC yaendelea kuongoza ligi ya Kanda ya Kati Zoni ya A

Mang’u Youth FC yaendelea kuongoza ligi ya Kanda ya Kati Zoni ya A

Na LAWRENCE ONGARO

MANG’U Youth FC ni miongoni mwa timu zinazolenga makubwa kwenye soka ya kuwania ubingwa wa mechi za Central Regional League (CRL), katika Kaunti ya Kiambu.

Sifa za timu hii zinatokana na umahiri wa kocha stadi Martin Mungai ambaye amekivumisha kikosi hiki kwa muda wa miaka mitano sasa.

Hapo awali kocha huyo alikuwa mshambulizi matata wa timu hiyo kabla ya kuanza kazi ya ukufunzi.

Kocha huyo anaeleza kuwa kikosi chake cha vijana 26 hufanyia mazoezi yao katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Mang’u, Gatundu Kaskazini kati ya Jumanne na Ijumaa.

Lengo lake kuu ni kuwahimiza vijana hao kuwa wavumilivu na kujituma kila mara wanapohudhuria mazoezi ili waendelee kuinua vipaji vyao.

Anasema mafanikio yoyote kwa mchezaji ni kuwa na nidhamu na kujituma mazoezini bila kushurutishwa.

Kocha huyo anakariri kuwa timu hiyo ina maono ya kuendelea kuwa timu bora miongoni mwa vikosi vya vijana stadi katika eneo la Mang’u na vitongoji vyake.

“Kila mara ninapowapa mazoezi uwahimiza wajiamini kwa kuonyesha kuwa wewe ni mchezaji stadi. Sio vyema kujiona eti huwezi kufika nafasi ya juu, lakini kuwa stadi ndiyo njia,” akafafanua Mungai.

Anaongeza kuwa ataendelea kuboresha kikosi hicho kwa kutafuta kila mbinu na njia za kuimarisha makali yake ili kuwa katika nafasi nzuri kwenye mashindano hayo.

Kwa wakati huu timu hiyo inakamata nafasi ya kwanza katika Kundi A kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ligi hiyo ya (CRL) ikiwa na pointi 37. Timu hiyo imecheza mechi 16 na kupata ushindi wa mechi 11 huku wakitoka sare nne.

Kocha huyo anamsifu nahodha wa kikosi hicho na mvamizi matata, Edwin Thuo, ambaye kwa ujuzi wake ameweza kufunga jumla ya mabao sita kati ya kumi ambazo wameweza kufunga. Hata hivyo alimpongeza kipa wao Simon Maina ambaye kwa ukweli amewaokoa kwa kunyaka michomo mikali langoni.

Kocha huyo anasema japo anatambua kibarua kilicho mbele yao ya kufanikiwa ni kigumu lakini ana imani vijana wake watajizatiti na kupiga hatua nyingine msimu ujao kwa kupanda hadi Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

Anasema kuorodheshwa katika michuano ya CRL msimu huu kulitokana na kutia bidii na kuwa miongoni mwa timu bora na kupata tikiti ya kushiriki michuano hiyo.

Anasema kila mchezaji ameonyesha ari ya kujituma ili kuhakikisha timu inamaliza katika nafasi nzuri msimu utakapoisha ili waingie katika kiwango kingine.

“Kidogo tumekuwa na shida katika safu ya ushambulizi lakini tumeanza kurekebisha makosa hayo huku wafungaji wetu wakianza kuziona nyavu,” anasema.

Meneja wa klabu hiyo Bw Linus Wambaki anasema wachezaji hao wamepewa nafasi ya kujitetea kila mara wakiona mambo hayaendi sawa.

“Jambo hilo limetupa mwelekeo mwema katika kikosi chetu kwa sababu kila mchezaji ana nafasi wazi ya kujitetea,” akafafanua meneja huyo.

Anasema jambo jingine linalowapa motisha ni kwamba mashabiki wanajitolea hata kuwafuata katika maeneo ya mbali wanaposafiri kwenda kucheza mechi za ligi.

You can share this post!

Wamaasai wataka operesheni Laikipia isitishwe

Mfumo wa kuinua uchumi bottom-up umetajwa kwenye Biblia –...