Manufaa ya kuendesha baiskeli

Manufaa ya kuendesha baiskeli

Na GEOFFREY ANENE

HUKU makundi mengi ya uendeshaji baiskeli jijini Nairobi yakiwemo Kenya Cycling na Wheels of Africa yakizidi kuhamasisha Wakenya kila mwezi kuhusu umuhimu wa kutumia usafiri huu, tovuti ya Taifa Leo ilikutana na Robert Maleya Azere ambaye amekuwa akitumia baiskeli kwa miaka 25, kufahamu kwa undani jinsi amenufaika.

Azere ni mmoja wa waendeshaji baiskeli zaidi ya 150,000 wanaominika kuishi katika kaunti ya Nairobi.

Robert Azere aelekea kazini akitumia baiskeli. Amefanya hii kuwa sehemu ya maisha yake tangu mwaka 1994. Picha/ Geoffrey Anene

Mkazi huyu wa mtaa wa Kariobangi South ana umri wa miaka 48.

Kwa karibu nusu ya umri wake, amekuwa akiendesha baiskeli kufika mahali pake pa kazi na kurejea nyumbani.

Yeye ni mhudumu wa stoo katika Taasisi ya Kitaifa ya YMCA katika eneo la Shauri Moyo.

Azere huendesha baiskeli kilomita 10 hadi mahala pake pa kazi na tena kurudi nyumbani kutoka Jumatatu hadi Jumamosi.

Amekuwa akifanya safari hizo kati ya Kariobangi South na Shauri Moyo kutoka mwaka 1994 yaani kwa miaka 25. “Nilinunua baiskeli ya aina ya Century mwaka 1993 na sijawahi kuibadilisha. Niliinunua kwa Sh2,000 kutoka kwa mkimbizi mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye alikuwa anahamia mjini Mombasa.

Bei yenyewe ya baiskeli hii ilikuwa Sh24,000, lakini kwa sababu hakuiona kama muhimu sana na pia alikuwa amepewa na Mzungu mmoja kama zawadi, akaamua kuniuzia kwa bei hii rahisi. Tangu niinunue nimefurahia manufaa yake.

“Kwa mfano, watu wanapolipa Sh70 kutoka Kariobangi South hadi Shauri Moyo na Sh70 kurudi, mimi naokoa fedha hizi kwa kuendesha baiskeli. Ukifanya hesabu, mimi kuokoa Sh840 kila wiki na zaidi ya Sh3,000 kila mwezi. Siathiriwi na msongamano wa magari kama wanaotumia magari. Natumia dakika 25 pekee kufika mahali pangu pa kazi na kati ya dakika 25 na 30 kurejea nyumbani.

“Fedha ninazookoa kwa kutolipia usafiri nalipa kodi ya nyumba nzuri na vitu vingine vinavyohitajika nyumbani,” anasema Azere, ambaye amekodisha nyumba ya Sh10, 000.

Baba huyu wa watoto watatu anasema uendeshaji wa baiskeli umemweka katika hali nzuri ya kiafya.

“Kuendesha baiskeli lazima ule vizuri,” anafichua kabla ya kuongeza, “Ni mazoezi mazuri sana ambayo yanakuweka fiti kimwili na hata kimawazo. Sina presha. Mara ya mwisho nilikuwa mgonjwa ilikuwa Agosti mwaka 2018 nilipopata mafua. Uendeshaji wa baiskeli ni mazoezi yanayokufanya uwe na nguvu.”

Kwa watu wanaopata mshahara mdogo, Azere anashauri, “Njia hii ya usafiri haiokoi tu muda unaotumia barabarani, bali pia fedha.”

Hakuna takwimu za kuonyesha watumiaji wa baiskeli kati ya Kariobangi South na Shauri Moyo kila siku, ingawa Azere anakadiria wameongezeka hadi 3,000 kutoka karibu 500 mwaka 1994.

Manufaa ya kuendesha baiskeli ni mengi. Mbali na yaliyotajwa na Azere ni kwamba uendeshaji wa baiskeli unasababisha majeraha machache zaidi kuliko njia nyingi za mazoezi.

Kuendesha baiskeli pia hakuhitaji ujuzi mkubwa.

Unapoelewa kuendesha baiskeli si rahisi usahau.

Vilevile, kunaimarisha afya ya moyo, nguvu za misuli, kusonga kwa viungo vya mwili na kunapunguza msongo wa mawazo na wasiwasi.

Uendeshaji wa baiskeli pia unafanya mifupa mwilini kuwa na nguvu na unaweza kupunguza matatizo mengi ya afya na masuala ya uzito wa mwili pamoja na unene wa kupitiliza.

Azere anakiri kwamba kuna changamoto kadhaa katika usafiri wa kutumia baiskeli. “Hakuna dawa kwa msimu wa mvua isipokuwa kutumia magari. Watumiaji wa baiskeli pia hawaheshimiwi barabarani. Gari linaweza kukupita na mara moja linasimama mbele yako. Usipokuwa na breki nzuri, bila shaka utaligonga na kuanguka na kuumia pamoja na baiskeli yako kuharibika bila ya kupata usaidizi wowote.”

Kuendesha baiskeli kwenye mabarabara mengi ya Kenya ni hatari kwa sababu mabarabara mengi yao hayana barabara maalumu ya baiskeli wala ya watu kutembea. Mengi yamejengwa kwa ajili ya magari pekee.

Kwa sababu hiyo, watu wanaotembea kwa miguu na kuendesha baiskeli wako katika hatari zaidi ya kuumizwa.

Vifo

Kulingana na Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama barabarani (NTSA), watu 16,948 wanaotembea kwa miguu na kuendesha baiskeli walipoteza maisha yao kati ya mwaka 2005 na 2014.

Sababu kubwa iliyochangia vifo hivyo ni kuwepo barabara chache zilizo na barabara maalumu ya waendeshaji baiskeli ambao wanalazimika kushindania barabara na magari. Mbali na hayo, waendeshaji wengi wa baiskeli hawavalii helmeti.

NTSA iliripoti Machi 14, 2019 kwamba watu wanaotembea kwa miguu ndio wako katika hatari zaidi ya kupoteza maisha kuliko watumiaji wengine wa barabara. Tangu mwaka 2019 uanze, watu 235 wanaotembea kwa miguu kati ya watu 630 waliopoteza maisha yao barabarani ni wale wanaotumia miguu. Takwimu za NTSA za tarahe hiyo zilionyesha kwamba vifo kutokana na uendeshaji wa pikipiki vimeteremka kutoka 136 hadi 127 katika kipindi sawa mwaka 2018.

Ushauri

Mnamo Machi 22, Muungano wa Automobile Association of Kenya, ambao una zaidi ya wanachama 100, 000 humu nchini, ulipiga jeki kampeni ya waendeshaji baiskeli kwa kuchapisha ujumbe muhimu kwenye ukurasa wa Facebook.

Taifa Leo imetafsiri ujumbe huo, “Watumiaji wengi wa mabarabara ni magari, waendeshaji wa pikipiki, waendeshaji wa baiskeli na watu wanaotembea kwa miguu. Kila mmoja wao ana haki ya kuwa barabarani. Kama dereva anayependa usalama barabarani, unahitaji kumpa mwendashaji wa baiskeli angaa nafasi ya mita 1.5 ama zaidi jinsi unavyompa dereva mwenzako. Tumia barabara kwa heshima.”

Ujumbe huu uliungwa mkono na waendeshaji wengi wa baiskeli akiwemo Otieno Lameck, ambaye alisema madereva wanawadharau sana barabarani.

“Haki vile motorists hutudharau sisi wenye baiskeli, they always hoot at us unnecessarilyI wish everybody would just be courteous enough on the roads (Madereva wanatudharau sisi waendeshaji wa baiskeli. Wanatupigia honi ovyo kila mara. Natamani kila mtu angeheshimu mwenzake barabarani).”

Uwekezaji

Mnamo Machi 7, 2019, viongozi wa mji wa Great Manachester nchini Uingereza walionyesha kuna manufaa makubwa kutumia baiskeli ama kutembea.

Walitangaza kwamba wataisukuma serikali ya Uingereza kuwekeza katika mradi wa uendeshaji wa baiskeli na matembezi.

Tovuti ya The Bolton News ilisema kwamba Meya wa mji huo Andy Burnham aliuliza Idara ya Usafiri kuipa uendeshaji baiskeli na matembezi umuhimu sawa na inavyowekeza katika mabarabara.

“Serikali baada ya nyingine zimekuwa zikichukulia uendeshaji baiskeli na kutembea kama vitu visivyofaa kupewa umuhimu. Hali hii haifai kuendelea wakati huu mabarabara yamejaa magari, kuna uchafuzi mkubwa wa hewa na viwango vya juu vya watu kutofanya mazoezi,” Meya huyo alinukuliwa akisema.

Bwana Burnham anatumai kwamba uwekezaji kutoka kwa serikali utapiga jeki mipango ya baraza la Greater Manchester Combined Authority (GMCA) ya kuwa na kundi la waendeshaji baiskeli na watu wanaotembea kwa miguu.

Gazeti la The Bolton News lilisema Greater Manchester inanuia kutumia Sh20.7 bilioni kufanikisha mradi huu.

Kamshina wa uendeshaji wa baiskeli na kutembea kwa miguu katika eneo la Greater Manchester, Chris Boardman alisema, “Lengo kubwa si kuendesha baiskeli tu, bali kuunda maeneo yanayoweza kuendeleza afya bora, ambayo yanaleta ustawi wa biashara, na yanawapa watu kitu mbadala na kuendesha magari. Maono yetu yanafaa kuungwa mkono kifedha jinsi sekta zingine za usafiri kama usafiri wa magari zinasaidiwa.”

Tazama picha zifuatazo za waendeshaji baiskeli:

Mwendeshaji baiskeli akiwa amevalia begi lenye rangi maalumu kwa ajili ya usalama barabarani. Picha/ Geoffrey Anene

 

Mwendesha baiskeli akiwa na bendera ya Kenya na jaketi la usalama jijini Nairobi. Picha/ Geoffrey Anene

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Mume wa mtu raha sana…’

Njaa: Wabunge wa ODM wamsuta Ruto

adminleo