Makala

Manufaa ya uvunaji maji

August 2nd, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

TIMOTHY Mburu, mzaliwa wa Kaunti ya Nyeri anasikitishwa na suala la maji kupotea hata msimu wa mvua.

Mkulima huyu ameiga mkondo wa Israel ambayo ni sehemu kubwa ni jangwa lakini inavuna tone lolote la maji kukiwa na mvua.

Kijiji cha Gitinga, Naromoru eneobunge la Kieni, Nyeri, ni miongoni mwa maeneo kame na yanayopokea mvua kiduchu.

Hata hivyo, katika shamba la mkulima Mburu, ni kiunga cha kilimo.

Katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne, Bw Mburu hukuza viazimbatata, kabichi na vitunguu saumu.

Ana bwawa lenye urefu wa futi 25 kuenda chini na linalositiri zaidi ya lita milioni 40 ya maji.

Limekalia katika kipande cha ardhi chenye ukubwa wa nusu ekari, ingawa maji yako kwenye robo ekari.

Kiini chake cha maji ni msimu wa mvua, ambapo mtaro wenye kimo cha karibu mita 500 urefu na futi mbili kuenda chini umeelekezwa bwawani.

“Kieni ni eneo kame, lakini uvunaji wa maji umegeuza shamba langu kuwa uga wa zaraa,” asema Bw Mburu, akiongeza kuwa shamba lake halikosi mavuno kila mwezi.

Mlima Kenya ni kiini cha mito inayoelekeza maji yake Mto Tana, na mkulima huyu anasema kilichomuatua moyo awali ni kuona maji yakipotea. Mkondo wa Mto Tana humiminia maji yake Bahar Hindi. “Kwa nini maji hayo yapotee ilhali yamepitia kaunti kadhaa, zingine zinazoshuhudia ukame na kukumbwa na njaa?” ashangaa Bw Mburu.

Ni wazo lililomsumbua tangu 2002 hadi 2004, wakati akisomea Stashahada ya Masuala ya Mazingira na Kilimomseto (Landscaping & Horticulture).

Licha ya kupata ajira, mkulima huyu wa aina yake anasema mapenzi yake yalikuwa tafakari ya namna ya kuvuna maji yaliyotoka Mlima Kenya pamoja na ya msimu wa mvua.

Mchakato wa uvunaji maji ulianza 2008 ambapo aliibuka na kampeni ‘tone la maji liwajibikiwe’ lililolenga kuteka maji msimu na mito ambayo kiini chake ni Mlima Kenya.

Bw Mburu anasema aliandikia Ubalozi wa Marekani pendekezo la uvunaji maji, na hata ingawa hakupata udhamini lilipitishwa. “Mwaka 2010 niliandika mapendekezo kadhaa kwa mashirika mbalimbali ya serikali na wadau husika ili kufanikisha wazo langu,” aeleza.

Mashirika aliyolenga ni; Halmashauri ya Nema, Warma, Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini-KWS na idara ya kilimo Kieni. Mkulima huyu anasema haikuwa rahisi kushawishi Nema kuhusu uchimbaji wa bwawa.

Mwaka mmoja baadaye, 2011, shamba lake lilipigwa msasa na akaruhusiwa kulichimba. Hatua ya kwanza ikawa kutafuta mwanakandarasi, ambapo bajeti ya shughuli zote ilitajwa kuwa kima cha Sh1.2 milioni.

“Niliweza kukusanya jumla ya Sh80, 000 kupitia mauzo ya mazao niliyokuza kupitia kilimo cha maji ya mvua, kuuza ng’ombe, mbuzi, vifaa vyenye dhamani vya nyumba na hata nguo,” adokeza.

Mkopo

Kupitia idara ya kilimo alipata mdhamini aliyempiga jeki kwa mkopo wa Sh400, 000.

“Pia ni kupitia idara hiyohiyo ambapo nilipata mdhamini mwingine aliyenipiga jeki kwa mkopo kuafikia Sh720, 000 zilizosalia kufanikisha uchimbaji wa bwawa,” anasema.

Aidha, lilichimbwa kwa trekta kwa muda wa siku 26. Ameliundia ukuta dhabiti na kulizingira kwa ua la nyaya.

Bw Mburu anasema mnamo 2012 aliacha kazi ya kuajiriwa ili kuzamia kilimo kikamilifu.

Wakati wa mahojiano aliambia Taifa Leo kwamba ilimgharimu Sh800 kununua mbegu za viazi. Shughuli za kuandaa shamba, upanzi na matunzo ndiye alijifanyia mwenyewe.

“Nilianza na thumuni ekari. Mavuno, nilipata magunia 10 yenye uzito wa kilo 110 kila gunia, moja likinunuliwa Sh6,000,” anafafanua.

Msimu wa pili, alipanua jitihada zake na kukuza viazi kwenye robo ekari.

“Msimu wa pili na tatu mazao yalikuwa bora,” anaeleza.

Amewekeza pakubwa katika kilimo cha viazi na kabichi.

Vilevile, hupanda vitunguu saumu na maharagwe aina ya minji, maarufu kama garden/garden peas. Hata hivyo, anasema vitunguu saumu alipania kufanya utafiti kuona iwapo vitakua eneo la Kieni, na amebaini vinafanya vyema.

Ana jenerata mbili za kupampu maji, na anazosema zimeimarishwa ili kupunguza gharama ya petroli.

Viazimbatata na ambavyo huvikuza kwa wingi, ameviratibia awamu sita kwa mwaka. “Upanzi huufanya kila baada ya miezi miwili,” Mburu asema.

Ili kupunguza gharama, huzalisha mbegu za viazi kupitia mfumo wa ‘true potato seeds’. Matunda ya miviazi maarufu kama ‘berries’, ndiyo huitumia kufanya shughuli hiyo.

Bw Meshack Wachira, mtaalamu wa masuala ya kilimo kutoka Novixa International Ltd, hata hivyo anasema mfumo huo unapaswa kufuatwa kwa umakinifu wa hali ya juu.

Kuna vigezo vinavyozingatiwa ili kuzalisha mbegu kupitia matunda hayo. Mimea inayovunwa mbegu zenyewe inapaswa kuwa na afya. Pia, iwe salama dhidi ya magonjwa na wadudu.

Tunda moja lina karibu mbegu 80, ambazo hukamwa na kukaushwa juani. Zinapandwa kwenye kitalu kwa muda wa miezi miwili ili kupata miche.

Kulingana na Bw Wachira ni kuwa miche hiyo hupandwa kama ipandavyo mboga. “Taratibu za maandalizi na upanzi ni sawa na za mboga,” aeleza mtaalamu huyu.

Timothy Mburu anasema miche ing’olewe na kuhamishiwa shambani kwa uangalifu. Siku 90, sawa na miezi mitatu, huwa tayari kwa mavuno, ambapo viazi vinavyovunwa ndivyo mbegu.

Wakati wa mahojiano katika shamba la Bw Mburu eneo la Naromoru, ilibainika mmea mmoja una uwezo wa kuzalisha karibu viazi 13.

Kando na kuzalisha mazao mbalimbali kupitia bwawa lake, lina samaki. “Limeongeza thamani ya shamba langu,” alisifia. Shamba lake ni uga wa mfunzo kwa wakulima jinsi ya kuvuna maji.