Michezo

Manyatta na Kitale Queens washindi wa Chapa Dimba

June 25th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KWA mara nyingine wawakilishi wa Mkoa wa Nairobi walishindwa maarifa na wapinzani wao katika fainali za kitaifa za ubingwa Chapa Dimba na Safaricom Season Two 2018/2019 kwa wavulana na wasichana.

Manyatta United (Mkoa wa Nyanza) na Kitale Queens (Mkoa wa Bonde la Ufa) zilitawazwa washindi wapya baada ya kutesa katika fainali zilizosakatiwa uwanjani Kinoru Stadium, mjini Meru. Baada ya mafanikio hayo timu hizo kila moja ilipongezwa kwa kitita cha Sh1 milioni na wadhamini wa kipute hicho kampuni ya Safaricom.

Manyatta United iliipepeta Al-Ahly ya Bonde la Ufa mabao 2-1 katika fainali. Nao warembo wa Acakoro Ladies (Mkoa wa Nairobi) walimaliza mbili bora baada ya kunyoroshwa kwa magoli 4-2 na Kitale Queens kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2.

Manyatta United iliyopigiwa chapuo kubeba taji hilo ilipata ushindi huo baada ya Mark Ochieng na Benson Ochieng kila mmoja kuitingia bao moja. ”Licha ya wapinzani wetu kuteremsha upinzani wa kufa mtu tuna furaha tele hatimaye tumetwaa ubingwa wa kitaifa mwaka huu,” golikipa wa Manyatta United, Nicholas Munangwe alisema.

Ali Nasri wa Super Solico (kulia) akishindana na mchezaji mpinzani wake, Elvis Muyale wa Lugari Blue Saints kwenye robo fainali za kitaifa za Chapa Dimba na Safaricom Season Two zilizopigiwa uwanjani Kinoru Stadium, Meru. Lugari Blue Saints ilishinda mabao 3-0. Picha/ John Kimwere

Kwenye nusu fainali Manyatta United iliikanyanga Lugari Blue Saints (Mkoa wa Magharibi) mabao 2-1 nayo Al-Ahly kupitia mipigo ya matuta ilivuna mabao 3-2 mbele ya South B United (Mkoa wa Nairobi).

Nayo Kitale Queens ilitafuna Barcelona Ladies kwa mabao 6-0 wakati Changamwe Ladies (Mkoa wa Coast) ikilala kwa mabao 4-2 mbele ya Acakoro Ladies.

Kwa tuzo za binafsi tuzo ya mchezaji anayeimarika (MVP) iliwaendelea Abdurahman Adullahi wavulana (Ah-Ahly) na Daisy Busia kitengo cha wasichana wa Kitale Queens.

Kitengo cha wavulana, Dennis Atsenga (Lugari Blue Saints), Mark Ochieng na Benson Ochieng wote(Manyatta) walituzwa wafungaji bora huku Jane Njeri wa Barcelona Ladies akibeba tuzo hiyo kwa wasichana.

Nao Nicholas Munangwe(Manyatta United) na Phyllis Chemutai (Kitale Queens) waliibuka mlinda bora kwa wavulana na wasichana mtawalia.