Manyota FC na Fafada kukutana fainali ya Sebe Legends Cup

Manyota FC na Fafada kukutana fainali ya Sebe Legends Cup

NA CHARLES ONGADI,

MSAMBWENI, KWALE

HATIMAYE michuano ya kuwania Sebe Legends Cup yalitinga hatua ya fainali baada ya mechi mbili za nusu fainali kupigwa mwishoni mwa juma iliyopita, Msambweni, Kwale.

Katika pambano la kwanza la nusu fainali, Viva Manyota FC ya Vingujini iliikomoa Dumna FC kutoka Mwaembe kwa mabao 5-4 kwa njia ya mikwaju ya matuta baada kuambulia sare ya 2-2 katika muda wa kawaida.

Katika mchuano huu uliogaragazwa uwanjani Nyumba Sita, Dumna ilitangulia kuona lango la Viva Manyota katika dakika ya 30 kwa bao la penalti lililopachikwa kimiani na Bakari Kiponda.

Lakini Viva Manyota FC chini ya mkufunzi wa zamani wa makipa wa timu ya Bandari FC, Rizak Siwa, ilipigana kiume na kusawazisha bao hilo katika dakika ya 43 kupitia Tumaini Bakari.

Timu hizi mbili zinazojivunia ushabiki mkubwa eneo hili, zilienda mapumzikoni zikiwa nguvu sawa ila kwa Bakari Kiponda kuiweka tena Dumna kifua mbele dakika ya 52.

Hata hivyo, Zakaria Hassan alisawazishia Viva Manyota bao hilo katika dakika 67 baada ya kumegewa krosi safi na Suleiman Pepe.

Baada ya muda wa kawaida kumalizika mwamuzi wa mchuano huu Bakari Mwariko aliamuri kupigwa kwa mikwaju ya matuta kubaini mbivu na mbichi baina ya timu hizi mbili.

Kabla ya kutinga katika hatua ya nusu fainali, Viva Manyota iliiduwaza Kidzumbeni FC mabao 2-1 uwanjani Maingidza. Nayo Dumna ikailemea Angola kwa magoli 4-3 kwa njia ya penalti katika mechi iliyochezwa katika uwanja huo huo.

Katika nusu fainali ya pili iliyochezwa siku ya jumapili uwanjani Mchinjirini, Fafada FC iliikwaruza Kings United mabao 2-1.

Mohammed Zakaria alitangulia kuiweka Fafada kifua mbele dakika ya 12 kisha Suleiman Rashid akaongeza la pili dakika ya 68.

Bao la kufutia machozi la Kings United lilisukumizwa kimiani na Mohammed Vuyaa kunako dakika ya 78 ya mchezo.

Kutokana na matokeo haya, Viva Manyota imeratibiwa kupepetana na Fafada katika fainali iliyoratibiwa kutandazwa mapema mwezi Aprili uwanjani Nyumba Sita, Msambweni kaunti ya Kwale.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti ya Nyeri yalenga kuchanja wanabodaboda 2,000

Vijana wahimizwa kjiunga na mafunzo ya Taekwondo