Habari

Maombi ya kuondoa mkosi wa ajali za mara kwa mara yafanyika Githurai 44

October 19th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

WAHUBIRI wa madhehebu mbalimbali eneo la Githurai 44, Nairobi wamefanya maombi ya pamoja ili kutakasa barabara ya Northern Bypass kufuatia ongezeko la mikasa ya ajali zinazoendelea kusababisha maafa.

Barabara hiyo ndiyo imeunganisha Ruaka, Kahawa West na Ruiru. Akizungumza na Taifa Leo, Kasisi wa kanisa la AIPCA, tawi la Githurai, Harison Kimaru amesema chini ya muda wa miaka miwili pekee eneo la Jordan-Budalangi limepoteza zaidi ya watu 50, ambao wamegongwa na magari.

Wenyeji wanalalamikia eneo hilo kutokuwa na matuta ya barabara kupunguza kasi ya magari kuwaruhusu kuvuka.

“Juma lililopita tulipoteza mtoto mwenye umri wa miaka 16 aliyegongwa na gari wakati akijaribu kuvuka. Eneo hili halina matuta, vyuma nguzo za barabara, wala mabango yenye alama za barabara kutahadharisha madereva,” akasema Bw Kimaru ambaye pia ni mwenyekiti wa mpango wa Nyumba Kumi eneo hilo.

Ukosefu wa ilani za barabara, vyuma nguzo na matuta, umetajwa kuchangia ajali na maafa eneo hilo. Picha/ Sammy Waweru

Alisema juhudi za kushirikisha viongozi eneo hilo akiwemo mbunge wa Roysambu, Waihenya Ndirangu, kupata suluhu zimegonga mwamba.

“Viongozi wetu na Halmashauri ya Barabara za Mijini (KURA), wote wametupa kisogo. Matumaini yetu sasa yapo kwa Mwenyezi Mungu na ndio maana tumeamua kufanya maombi kuitakasa,” Kasisi huyo akaelezea, wakati wa maombi hayo yaliyohusisha zaidi ya wahubiri 20.

“Tumekuwa tukifunga na kuombea barabara hii mikasa ya ajali ituondokee kwa sababu tumepoteza wengi kupitia ajali,” akasema Pasta Lucy Shama.

Kasisi wa kanisa la AIPCA, tawi la Githurai, Harison Kimaru na aliyeongoza wahubiri hao. Picha/ Sammy Waweru

Wakati huohuo madereva wametakiwa kuwa waangalifu na waadilifu wakiwa barabarani, utepetevu wa baadhi yao ukitajwa kama kisababishi kikuu cha maafa yanayoshuhudiwa.

“Kwa madereva watumizi wa Northen Bypass, uadilifu na umakinifu mkiwa barabarani ndio utasaidia kupunguza ajali na maafa,” akahimiza Askofu Margaret Karanja.

Kulingana na wakazi ukosefu wa ilani za barabara, vyuma nguzo na matuta, pia umechangia magari yanayopoteza mwelekeo kuharibu nyumba zao.

Northen Bypass ni barabara yenye shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi.