Makala

Maombi ya saa moja yaliyomfanya Omosh akaacha pombe na kuokoka 

April 16th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MUIGIZAJI wa zamani Joseph Kinuthia almaarufu Omosh, ameelezea jinsi Mungu alivyomwongelesha akimuahidi kumsaidia kuachana na pombe, mihadarati na sigara.

Kulingana na msanii huyu aliyekuwa akiigiza katika kipindi cha Tahidi High – Cha runinga ya Citizen, pombe na matumizi ya dawa za kulevya na sigara, haina starehe.

Kwake sasa, ni kukosa kuelewa na waliotekwa na kero hiyo hatua hiyo akiitaja kama ‘ujinga tu’.

“Hakuna ushujaa ndani ya uraibu wa pombe, mihadarati na sigara. Ni upumbavu tu,” anasema.

Omosh alijijengea jina kupitia maigizo Tahidi High japo kabla ya kuwa na ukurasa mpya wa maisha alikiri kulemewa na pombe.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali kwa njia ya simu, alikiri jinsi Januari 9, 2023 Mungu ‘alimuandama na kumpa afueni maishani’.

“Hiyo ndiyo siku nilikiri uwepo wa Mungu na nikamwambia kwamba leo ni leo, lazima unipe mbinu kurekebika kabisa katika haya ya kujiharibu,” alisema.

Alifichua kwamba alikuwa ameachana na pombe mwaka wa 2022, lakini uvutaji sigara ukawa bado umemkalia ngumu asiweze kuukoma.

Lakini Januari 2023 alifanikiwa kumlilia Mungu kiasi kwamba “niliamua kuokoka na Mungu wangu kwa sauti akaongea nami na akaniambia nimesikia kilio chako, umekuwa mshindi na nimekuponya”.

Anasema maombi yake kwa Mungu yalianza saa nne asubuhi na yakachukua saa moja “machozi ya kutubu yakinitiririka kama chemichemi ya maji”.

Anasema Mola alimkumbusha jinsi alivyozaliwa katika familia ya wacha Mungu, akitamani kuafikia makuu ya kimaisha ndani ya tabia njema.

“Katika kutafakari, niliamua kwamba lazima ningerekebisha mienendo hata ikiwa sio kwa nia ya kuwa tajiri, ili maisha yangu yawe ndani ya ngome ya wokovu,” anasema.

Kwa sasa, Omosh ameajiriwa katika karakana ya mbao mjini Kikuyu, Kaunti ya Kiambu akiwa na ushuhuda wa jinsi ulevi huathiri maisha ya binadamu kiasi cha kumpotezea mianya ya kujiendeleza, kukosea mtu heshima na kuyumbisha afya.

“Kwa kunywa pombe, yalikuwa maamuzi ya kurejesha nyuma maisha yangu,” akaambia Taifa Dijitali.

Alisema kwamba maisha yake ya ulevi yamejaa kumbukumbu za masikitiko, na kwa sasa anaweza akasimama wima na kwa kipaza sauti atangazie wote kwamba “hakuna ushujaa utakuwa nao ndani ya ulevi, hali itaishia ujinga usipobadili mienendo”.

Bw Omosh alisema kwamba aliachana na ulevi mwaka wa 2022 baada ya kuzama ndani ya mtindi kwa zaidi ya miaka 30.

“Ina maana kwamba nilihujumu zaidi ya asilimia 50 ya maisha yangu ndani ya ulevi. Nilitoka tu na majina ya majazi yasiyo na faida kamwe, jina kubwa na sifa tele lakini bila mwelekeo wowote wa kimaisha,” akasema.

Omosh alifichua kwamba kanisa lake ambalo humlisha chakula cha kiroho tangu aokoke ni la Redeemed Gospel, Komarock, Jijini Nairobi.

Anasema kwamba maisha yake yalianza kwenda mrama wakati alijuana na marafiki wa kumweka kombo badala ya kumjenga.

“Nikitafakari kuhusu maisha yangu hadi sasa, mimi huwa na masikitiko kwa kuwa nilitekeleza maamuzi yasiyo ya busara na nilikuwa nikisuta wote waliokuwa wakiona hali ya tahadhari ndani ya maisha yangu kama wasiojua walichokuwa wakinikanya nikome,” asema.

Anasema kwamba akiwa ndani ya ulevi, alikuwa akitekeleza maamuzi hata ya mauti, yakiwemo kuendesha gari kwa mwendo wa kasi, kubugia pombe aina zote pasipo kipimo na pia uvutaji sigara na bangi.

“Hali ni kwamba, nilipoteza mianya ya kujiendeleza, na ningekuwa mbali sana katika haya maisha. Lakini kwa kuwa sikuwajibika, niko vile nilivyo lakini nikiwa na amani tosha ya kujuana na Maulana kama Mwokozi wa maisha yangu na ambaye hunipa kitulizo,” asema.

Anasema alizama ndani ya deni zisizofaa, jina lake kubwa na talanta ya kipekee zikigeuka kuwa maadui ya kujiangamiza badala ya kuwa chombo cha kumpa maisha bora.

Anasema ulifika wakati ambapo alisombwa na mawazo na akaanza kuishi maisha sawa na ya walio na akili punguani, lakini kimiujiza akapona tu.

Bw Omosh anasema kwamba “jumba ambalo nilijengewa na mhisani liko tu na sijaliuza kama ilivyotangazwa mitandaoni”.

Lakini alisema kwamba sababu zake za kutolitumia ni zake binafsi na wakati muafaka ukifika, ataliingia tu lakini akionya kimafumbo kwamba “hali yangu ya awali imejaa uongo mwingi sana na ambao kwa sasa nimeukoma”.

Anasema kwamba tangu amkubali Yesu kama Mwokozi wa maisha yake, amepata afueni kuu kiasi kwamba hata amekumbatia familia yake ambayo alikuwa ameipa talaka.

“Mimi ningekusihi kwa dhati uachane na ulevi, koma mihadarati na uachane na sigara kabisa… Koma ulevi wa aina yoyote ule. Mimi nakwambia hivyo nikiwa nimepitia masaibu ya ulevi na nikapata ushuhuda wa moja kwa moja. Uking’ang’ania kuwa mlevi utaishi na majuto kama mjukuu,” asema.

[email protected]