Maoni

MAONI: Bado tuna kibarua kukabili mabadiliko ya tabianchi

May 1st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MIONGO kadhaa iliyopita, ilikuwa vigumu sana kumsikia mtu akizungumzia suala la mabadiliko ya hali ya hewa.

Lilikuwa suala geni, kwani athari zake hazikuwa zimeanza kudhihirika.

Nyakati hizo, maeneo mengi nchini bado yalikuwa na kiwango kikubwa cha misitu. Mito ilikuwa yenye maji mengi na safi yaliyokuwa yakitumika na wanavijiji kwa shughuli zao za kila siku.

Maji katika mito mingi yalikuwa yakitoka kwenye chemchemi zilizokuwa katika maeneo ya misitu na milima.

Katika vijiji vingi, ilikuwa nadra kumsikia mtu akilalamika kuhusu njaa -kwani chakula kilikuwepo kwa wingi nyakati zote.

Misimu pia ilikuwa ikifuatana kama kawaida. Kwa mfano, mvua ya masika ilikuwa ikinyesha kati ya Machi na Mei huku msimu wa mvua chache ukiwa kati ya Oktoba na Novemba.

Hata hivyo, baada ya athari za mabadiliko ya hewa kuanza kushuhudiwa katika sehemu tofauti duniani, kila kitu kilionekana kuanza kubadilika. Mkondo wa misimu ulibadilika, huku kiwango cha mvua ambacho kilikuwa kikinyesha pia kikibadilika.

Kwa mfano, katika msimu ambao mvua ilihitajika inyeshe kwa uchache, ilianza kunyesha kwa wingi, kwa kiwango cha kusababisha mafuriko na hata maafa!

Katika msimu ambao mvua ilitakikana inyeshe kwa wingi, inakosa kunyesha kabisa! Badala yake, msimu huo unabadilika kuwa wa kiangazi kikali.

Bila shaka, mabadiliko hayo ya misimu yalileta madhara makubwa kwa maisha ya wanadamu na wanyama. Mabadiliko hayo ndiyo yamekuwa chanzo cha maafa yanayotokana na hali ya njaa na misimu isiyoisha ya kiangazi.

Urejeleo huo, bila shaka, unaangazia hali tunayoshuhudia nchini kwa sasa, ambapo zaidi ya watu 70 wamefariki kutokana na mafuriko yanayotokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Ukweli ni kuwa, kwa namna moja mafuriko hayo yanatokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Haya ni maelezo ambayo yametolewa na wadau wengi wa kimazingira ambao wamekuwa wakifanya tafiti zao kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.

Akiwa mwanasayansi, Rais William Ruto pia ameonyesha kujitolea kwake katika kuwahamasisha raia kuhusu athari za kimazingira za mabadiliko ya hali ya hewa.

Mara tu alipochukua uongozi, Rais Ruto na viongozi wengine walianza harakati za kuongoza shughuli za upanzi wa miti katika sehemu tofauti nchini.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa juhudi hizo hazitoshi hata kidogo. Hatua nyingi bado zinafaa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa kwa pamoja, Kenya imeshinda vita vya kudhibiti athari hizo.

Kama kiongozi wa mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo katika Umoja wa Afrika (AU), Rais Ruto anafaa kutumia nafasi yake kuwahamasisha viongozi wengine barani kufuata nyayo za Kenya, ili kuhakikisha Afrika imeepuka majanga kama mafuriko na kiangazi.