Maoni

MAONI: Benny Hinn aliacha nchi hoi badala ya kuiletea uponyaji

March 1st, 2024 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

MHUBIRI Toufik Benedictus Benny Hinn alikuwa gumzo humu nchini wikendi iliyopita alipoongoza mkutano mkubwa wa maombi ya ‘kuponya nchi’ uwanjani Nyayo, Nairobi.

Mhubiri huyo wa Amerika-Canada alikuwa amealikwa na serikali ya Kenya ‘kuponya nchi’.

Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, Benny Hinn ameacha Kenya ikiwa imelemewa na maradhi zaidi kuliko alivyoipata.

Ili kubaini ikiwa Benny Hinn aliponya Kenya au la, tunahitaji kupiga darubini ni maradhi yapi yanahangaisha Kenya.

Miongoni mwa maradhi sugu yanayohangaisha Kenya ni ufisadi, ukabila, umaskini, ufujaji wa fedha za umma, uongozi mbovu, mapuuza ya maagizo ya mahakama, vigogo wa serikali kuteka asasi huru kama vile Idara ya Polisi, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP); na wanasiasa kuwapa wapigakura ahadi hewa wakati wa uchaguzi.

Kwanza, mkutano wa Benny Hinn ulichangia katika moja ya maradhi hayo – ufujaji wa fedha za umma kuandaa mkutano huo.

Mamilioni ya fedha zilitumika kuweka mamia ya mabango kila kona ya jiji la Nairobi na kukodisha malori na watu wa kuzunguka jijini wakishawishi wakazi kuhudhuria maombi hayo ya ‘uponyaji’.

Japo Mkewe Rais, Rachel Ruto, alisisitiza kwamba mkutano huo ulifadhiliwa na makanisa, dalili ni wazi kama meno ya ngiri kwamba, fedha za umma zilitumika.

Miezi mitano iliyopita, Benny Hinn alifichua kwamba, alialikwa na Mkewe Rais kuongoza mkutano wa injili ambao ungefadhiliwa na serikali ya Kenya.

Mhubiri huyo alisema hii ilikuwa mara ya pili kwake kualikwa na serikali ya baada ya Papua, Indonesia.

Ikiwa kweli mkutano huo ulifadhiliwa na viongozi wa makanisa, ina maana kwamba “mtumishi wa Mungu” Benny Hinn alidanganya kwamba ungefadhiliwa na serikali.

Viongozi wote wa serikali wakiwemo Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walihudhuria mkutano huo – ishara kwamba haukuwa wa kawaida. Kiongozi wa Nchi alivalia suti inayofanana na ile ya Benny Hinn. Huo ni ushahidi kuwa kulikuwa na mawasiliano ya karibu baina ya mhubiri huyo na Ikulu.

Waziri wa Huduma za Umma Moses Kuria alinukuliwa akisema mkutano huo ulikuwa wa serikali.

Hatua ya Benny Hinn kuingilia mzozo wa Palestina na Israeli pia ilipaka Kenya tope kama nchi inayounga mkono mauaji yanayoendelea katika ukanda wa Gaza. Waziri Kuria alilazimika kumkemea huku akisema kuwa Kenya haiungi mkono mauaji hayo.

Benny Hinn pia ameacha wahubiri wa humu nchini walioenda ‘kupokea nguvu za uponyaji’ kutoka kwake uwanjani Nyayo wakiwa taabani.