Maoni

MAONI: EACC iwe tayari kupambana na wezi wa pesa za mafuriko

May 9th, 2024 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

BAADA ya dhiki ni faraja. Msemo huu unalenga kutia moyo watu wanaopitia dhiki –kama vile waathiriwa wa mafuriko ambao wamepoteza mali na hata kulazimika kuhama makazi yao –kwamba katika siku za usoni watarejelea hali yao ya kawaida.

Lakini nchini Kenya, msemo huo una maana nyingine kuwa dhiki huleta faraja kwa mafisadi katika serikali za kaunti na kitaifa.

Mabilionea wapya nchini Kenya huibuka baada ya majanga yanyosababisha dhiki kama vile mafuriko au mkurupuko wa magonjwa kama vile Covid-19.

Baada ya janga la Covid-19 lililokumba nchi kati ya 2020 na 2021, kulijitokeza kundi jipya la mabwanyenye waliopachikwa jina la ‘mabilionea wa Covid-19’.

Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF) na Mkaguzi wa Matumizi ya Fedha za Umma wanashuku kuwa sehemu kubwa ya Sh173 bilioni zilizofaa kutumika kupambana na makali ya maradhi ya Covid-19, ziliishia katika mifuko ya wachache katika Taasisi ya Kununua na Kusambaza Dawa nchini (Kemsa) na serikalini.

Hospitali zilikosa vifaa muhimu vya matibabu kama vile oksijeni ilhali ‘mabilionea wa covid’ wakiogelea kwenye utajiri.

Janga la mafuriko ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 250 humu nchini na wengine maelfu kupoteza makazi na mali yao, limetoa mwanya kwa mafisadi kujitokeza tena.

Baada ya miezi kadhaa sakata ya ‘mabilionea wa mafuriko’ itajitokeza kwani wafisadi hawana utu.

Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) ya hivi karibuni inaonyesha kuwa serikali za kaunti hazijatumia jumla ya Sh973 milioni ambazo ni sehemu ya Sh1.9 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mikasa na majanga katika mwaka wa matumizi ya fedha wa 2023/2024.

Mafuriko yametoa mwanya kwa wafisadi katika kaunti ‘kutafuna’ fedha hizo huku waathiriwa wakiendelea kuhangaika.

Mnamo 2015, Wakenya walipigwa na butwaa serikali ilipotenga Sh37.5 milioni kununua sabuni 1,000 kwa ajili ya waathiriwa mafuriko yaliyokuwa yametabiriwa kuwa yangesababishwa na mvua ya El Nino.

Mvua hiyo, hata hivyo, haikunyesha lakini mamilioni yalitoweka katika serikali za kaunti na kitaifa wakidai kuwa tayari walikuwa wametumia sehemu ya fedha kufanya maandalizi ya kupambana na mafuriko.

Rais William Ruto wiki iliyopita alitangaza kuwa kila familia iliyoathiriwa na mafuriko itapewa Sh10,000 ili kuziwezesha kukidhi mahitaji ya chakula, kodi ya nyumba na kadhalika.

Kuna hofu kwamba fedha hizo huenda zikafikia familia chache na kiasi kikubwa kuishia kwa mifuko ya wachache serikalini ambao wataibuka kuwa mabilionea baada ya mafuriko.

Wahisani pia wamekuwa wakitoa misada kuwezesha serikali kupambana na janga la mafuriko ambalo limeathiri zaidi ya kaunti 20. Fedha hizo za wahisani pia ziko katika hatari kubwa ya kuibwa na wafisadi.