Maoni

Hivi huyu Raila ana nyota kweli, au kidagaa kitamuozea pia huko AUC?

April 13th, 2024 2 min read

NA DOUGLAS MUTUA

USIINGIE baridi unapoona mataifa mengine yakijitokeza kumpinga Bw Raila Odinga, anayewania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC). Hilo lilitabirika tangu mwanzo.

Maoni yangu ya kwanza Bw Odinga alipotangaza kuwa angewania wadhifa huo yalikuwa kwamba tusisherehekee mapema.

Nilikuwa mumu humu tulipojiandaa kwa hamu na ghamu kushuhudia Kenya ikitawazwa mshindi katika kinyang’anyiro sawa na hicho, ila tukaambulia patupu mnamo 2017.

Wakati huo, tulisalitiwa na majirani zetu wa Afrika Mashariki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bi Amina Mohammed, akabwagwa kishenzi na mwaniaji kutoka Chad, Dkt Moussa Faki Mahamat.

Si kwamba Dkt Mahamat alikuwa maarufu kote barani Afrika, au eti alikuwa na tajiriba kubwa kumpiku dada yetu Amina, la hasha! Amina hakuwa na nyota.

Je, Raila ana nyota? Ni vigumu sana kutabiri, hasa kwa kuwa wadhifa anaotafuta hautegemei umaarufu wa mtu binafsi bali taifa lake linalomfadhili.

Swali tunalopaswa kujiuliza ni iwapo Kenya ni maarufu ndani na nje ya bara la Afrika kiasi cha kuyashawishi mataifa mengi kumchagua Bw Odinga badala ya wapinzani wake wawili kutoka Somalia na Djibouti.

Nimesema nje ya Afrika kwa kuwa kila kinachoendelea katika uongozi wa AU hupata ushawishi kutoka Amerika, Uropa, Uchina, Urusi na kwingineko.

Nimetazama uwaniaji wa Bw Odinga kwa jicho la tatu baada ya kuona kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Bw Mahmoud Ali Youssouf, ameingia ulingoni pia.

Hadi kufikia kujitokeza kwa Bw Youssouf, mpinzani wa pekee wa Bw Odinga alikuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Somalia, Bi Fawzia Adam.

Tuambizane ukweli: Hakuna tofauti kubwa kati ya Somalia na Djibouti; watu ni wamoja, utamaduni wao mmoja, dini ni moja – Uislamu – na hata lugha ya kiasili ni moja tu – Kisomali. Tofauti ndogo iliyopo ni kwamba, lugha ya kigeni inayonenwa Djibouti ni Kifaransa, huku Somalia wakizungumza Kiingereza, japo cha kuombea maji.

Katika akili za mtu yeyote aliye na asili ya Somalia – na hapa nakutolea mifano ya watu kama Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Bw Aden Dualle, Bi Mohammed na wengineo – Somalia ni ‘taifa’ moja pana lisilodhibitika ndani ya mipaka ya nchi tatu wanakopatikana kwa wingi.

Aghalabu uzalendo wao upo kwenye ‘taifa’ hilo moja la kufikirika, si wanakodai kuwa na uraia, hivyo ni rahisi kwao kuungana likizuka la kuwaunganisha kimataifa.

Usione ajabu iwapo wawaniaji hao wa Somalia na Djibouti watafanya kampeni kwa fujo kuu kote Afrika, uchaguzi ukikaribia mmoja ajiengue, amwachie mwenzake kupambana na Bw Odinga!

[email protected]