Maoni

Hivi unajua urais mwingine wa Trump utakuwa na athari gani kwa Mwafrika?

April 5th, 2024 2 min read

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI aliyekuwa Rais wa Amerika, Donald Trump, akichaguliwa tena, atakuwa na athari gani kwa Mkenya au Mwafrika kwa jumla?

Nauliza kwa kuwa kuna dalili kwamba, huenda akauwahi wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba mwaka huu.

Ikiwa nimewahi kukuhakikishia kuwa Trump hatachaguliwa tena, sahau niliyokwambia, uzingatie unayosoma hapa sasa hivi.

Sikukuhadaa makusudi, moyo wangu ulikuwa safi, ila kama mwanadamu yeyote yule, nina mapungufu yangu, hivyo kugonga ndipo na kunoa, yote yamo maishani mwangu.

Maoni yangu hayo yalitoka moyoni, tena baada ya kutilia maanani masuala tofauti-tofauti tu ambayo yakiendelea kwenye uga wa siasa nchini humo, lakini sasa hata nami nimeanza kuwa na shaka.

Profesa fulani hupenda kuniambia kuwa, Trump anaandamwa na roho wa Mpinga Kristo anayeelezewa kwenye Biblia, yaani hashindiki kwa chochote, na kila mkisubiri aanguke na kufedheheka ili msherehekee, mnafedheheka nyinyi.

Mashtaka mengi yanayomkabili yanaonekana kuheshimu ushawishi wake hivi kwamba, takriban kila mchanganuzi wa siasa anasema ni vigumu Trump kufungwa gerezani kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Miongoni mwa mashtaka mabaya zaidi ya jinai yanayomkabili ni la kuiba nyaraka rasmi za serikali kutoka Ikulu ya White House baada ya kushindwa na Rais Joe Biden mnamo 2020.

Hata hivyo, huenda kesi hiyo ikajikokota hadi baada ya uchaguzi ujao kwa kuwa mwongoza-mashtaka na jaji anayeishughulikia wanazozana, jaji akituhumiwa kumpendelea Trump.

Mwanasiasa huyo matata ana wafuasi wanaompenda ajabu, hivyo ana hakika watajitokeza kwa wingi kumchagua. Hatuwezi kusema hivyo kumhusu Rais Biden, ambaye, licha ya kuendesha nchi kwa utulivu na kukuza uchumi vizuri tu, hawachangamshi wengi.

Wengi wanasingizia uzee wa Biden, ila hata Trump ni mzee anayenusa miaka 80, hivyo kuna kitu ambacho Trump anakifanya na kuwavutia watu wengi.

Kura za maoni za hivi punde zaidi zinaonyesha kuwa, katika majimbo saba yanayotarajiwa kumpa au kumnyima mtu ushindi, Trump anamshinda Biden kwa majimbo sita! Ikiwa takwimu hizo ni za kuaminika, si kama za Kenya, sasa unajua Trump yuko kifua mbele.

Alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2016, Waafrika wengi walitania kwamba angaliwarejesha nyumbani wajomba na mashangazi zao waliopotelea Marekani.

Ikizingatiwa kwamba Trump akishinda uchaguzi atatumika kipindi chake cha mwisho, hivyo hatahitaji kuwafurahisha watu, inatabirika kuwa athari za utawala wake ndani na nje ya mipaka ya Marekani zitadumu miongo mingi.

[email protected]