Maoni

MAONI: Matabibu ni muhimu ila wasichangie udunishaji wa wataalamu wengine

May 10th, 2024 2 min read

NA MARY WANGARI

MGOMO wa madaktari ambao umedumu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa umeibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya huku mamia ya wagonjwa wakiendelea kuteseka.

Wakenya wanaougua maradhi sugu kama vile saratani, figo, kisukari, shinikizo la damu na mengineyo, wamepitia masaibu yasiyoweza kuelezeka na hata wengine kupoteza maisha yao baada ya sekta ya afya nchini kulemazwa kabisa.

Familia zimebaki na machungu baada ya kuwapoteza wapendwa wao hata baada ya kujitahidi juu chini kuwaokoa bila mafanikio hasa ikizingatiwa ni Wakenya wachache wanaweza kumudu huduma ghali za matibabu katika hopsitali za kibinafsi.

Kinaya ni kuwa, madaktari wao hao wanaosusia kuwahudumia wagonjwa katika hospitali za umma walipoajiriwa na serikali, ndio wanaoendesha kliniki na hospitali nyingi za kibinafsi yakiwemo maduka ya kuuzia dawa.

Ni katika kipindi hiki ambapo kulizuka mdahalo wa kustaajabisha ulioonekana kusawiri taaluma kama vile udaktari kuwa muhimu zaidi kushinda nyinginezo.

Baadhi ya wanasiasa hata walijitokeza hadharani kuwadhalilisha wauguzi wanaofanya kazi kwa karibu na madaktari, hatua iliyohatarisha utoaji wa huduma ya afya hasa ikizingatiwa kazi muhimu wanayofanya ya kuwatunza wagonjwa.

Japo ni suala tata ambalo wengi wanajiepusha kuzungumzia, wakati umewadia kwa serikali kufanyia marekebisho mfumo unaotumika kuwalipa madaktari.

Sawia na inavyofanyika katika nchi zilizoendelea, madaktari wanafaa kulipwa kulingana na saa walizofanya kazi ili kuboresha utoaji huduma na kupunguza visa vya utepetevu wa wahudumu wa afya katika hospitali za umma.

Huku madaktari wakitaka wanagenzi kulipwa mshahara wa zaidi ya Sh200,000, walimu wa Sekondari ya Msingi (JSS) walijitokeza wakilalamikia vikali kulipwa mshahara wa Sh17,000.

Ukweli ni kwamba, wataalam wote wawe ni wauguzi, wakunga, walimu, majaji, wahandisi, mawakili, wanahabari na wengineo wana mchango muhimu katika jamii. Wanastahili heshima na haki ya kulipwa mshahara unaowawezesha kujikimu kimaisha hasa baada ya kutia juhudi kielimu na kufuzu kufanya kazi hizo anuai.

Iwapo tutatumia kipimo cha werevu kuhusu alama au idadi ya miaka inayotumika kuwa daktari, wahandisi tunaowategemea kujenga majumba tunayoishi, barabara na madaraja ya kusafiria ikiwemo mitambo na mashine ya matibabu na mengineyo, wanahitajika vilevile kupata alama za juu na kutumia zaidi ya miaka mitano wakisomea taaluma hiyo.

Kuna Wakenya wanaotumia vipaji vyao kama wasanii, wachezaji kabumbu na wanariadha tajika na wameliweka taifa letu kwenye ramani ya dunia na kuvutia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.

Jaribio la kusawiri baadhi ya taaluma kuwa muhimu kuliko nyingine halina msingi wowote na linapaswa kukemewa vikali kwa sababu linatishia kuzua uhasama wa kitaaluma na hata kuhatarisha ndoto za maelfu ya watoto wanaorauka kila uchao wakiwa na matumaini ya kuwa na maisha bora.

[email protected]