Habari Mseto

Maoni mbalimbali yazidi kutolewa kuhusu ripoti ya BBI

December 3rd, 2019 3 min read

Na MISHI GONGO na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI kutoka Kaunti ya Tana River wamewaomba wakazi kuwapa muda kuichambua ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kuona kama ina faida kwa wakazi hao kabla ya kusema ikiwa wanaiunga mkono au vinginevyo huku katika Kaunti ya Kiambu baadhi ya viongozi wakiwasihi wakazi kujisomea wenyewe.

Wakiongea katika shule ya Ngao ambako walikuwa wamehudhuria hafla ya harambee kuchangisha pesa za ujenzi katika shule hiyo, walisema wanataka kuhakikisha kuwa ripoti hiyo haitaathiri uchumi wa wakazi wa Tana River kabla ya kutangaza msimamo wao.

Viongozi hao wakiongozwa na mwakilishi wa wanawake Bi Rahema Hassan na aliyekuwa mbunge wa Garsen Danson Mungatana, pia waliwataka wakazi hao kutojiunga na mrengo wowote hadi pale viongozi hao watakapo weka kikao kujadili mrengo utakao waletea maendeleo.

“Tunataka kuichambua ripoti hii kuhakikisha kuwa inamanufaa ya kibiashara na hata uchumi,hatutaki kupitisha jambo ambalo litakuwa linawakandamiza wananchi,” alisema Bw Mungatana.

Kauli yake hiyo iliungwa mkono na Bi Hassan ambaye aliwaonya wakazi dhidi ya kutumiwa na viongozi walio na tamaa ya kujinufaisha wao binafsi.

“Tumechoka kutumiwa na viongozi wabinafsi wanaotaka kujilimbikizia mali kwa kutumia wananchi wa kawaida. Hata sisi tunataka sauti yetu isikike kuhusiana na ripoti hii,” alisisitiza Bi Hassan.

Alisema wataandaa kikao na viongozi wote wa Tana River na kutafuta wataalamu ambao watawasaidia kuchambua ripoti ya BBI kabla ya kutangaza msimamo wao.

Aidha, aliwataka wabunge kuwapa wananchi muda wa kutosha kuchambua ripoti hiyo ili wafanya maamuzi ya msingi.

Kwingineko, spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi yuko katika hatari ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani iwapo mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria atatekeleza tishio lake la kupeleka mswada bungeni akimshutumu spika huyo kwa kuchukua msimamo wa mapema katika suala la ripoti ya BBI na kupuuzilia mbali wanaotaka kupeleka ‘suala’ hilo bungeni.

Ripoti ya BBI tayari imezua tumbojoto miongoni mwa wafuasi wa kiongozi wa ODM na wale wa Naibu Rais William Ruto tangu kutolewa kwake wiki iliyopita.

BBI ambayo waasisi wake wanasema inalenga kuwaleta Wakenya pamoja imesababisha kuwepo mjadala mkali na viongozi mbalimbali nchini.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema Ijumaa anaiunga mkono ripoti ya BBI lakini akawashauri wananchi wawe mstari wa mbele kuisoma ripoti hiyo kwa makini ili kila mmoja awe na maoni yake kamili.

“Tungetaka kuona kila mmoja wetu akichukua jukumu la kujisomea ripoti hiyo kwa makini ili baadaye asije kupotoshwa kufanya maamuzi yasiyofaa,” alisema Bw Wainaina.

Hata hivyo, alisema licha ya kuiunga mkono, hakubaliani na mtindo wa kutaka kugawanya mamlaka kwa viongozi wachache.

“Ripoti hiyo kwa hakika inaangazia maswala mengi muhimu yanayoweza kunufaisha mwananchi wa kawaida lakini hata hivyo kila mmoja anastahili kutoa maoni yake bila kushinikizwa kufuata ya mwingine,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo Ijumaa wiki jana akiwa eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki, hafla ya mazishi ya watoto wawili walioangamia katika ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Thika-Kenol iliyofanyika juzi.

Utangamano

Naibu gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema siku ya kitamaduni ni muhimu kwa nchi kwa sababu inaleta utangamano miongoni mwa wananchi.

“Huu ndio wakati wa kila mmoja kujitokeza na kujisomea ripoti hiyo ili baadaye watu wajiamulie ni jambo lipi wanalolitaka kupitia ripoti hiyo,” alisema Dkt Nyoro.

Alitoa pendekezo siku ya Januari Mosi, itambuliwe kama siku ya Utamaduni.

Bw Stephen Ndicho ambaye ni spika wa bunge la Kaunti ya Kiambu, alisema siku ya Desemba 26 ni ya ‘Boxing Dei’ huadhimishwa na Wakristo wote ulimwenguni.

Hata hivyo pia alipogeza mpango wa kuwepo siku ya Utamaduni nchini lakini alipendekeza itafutiwe tarehe nyingine tofauti.

Wakazi wengi wa Kiambu waliohojiwa walisema tayari wameisikia ripoti hiyo na kile kilichosalia ni kuketi chini kwa makini na kujisomea ili kutoa uamuzi unaofaa kwao.

“Mimi nitafanya juhudi nijaribu kuisoma halafu baadaye nitatoa maoni yangu. Wakati huu sio wa kusomewa na yeyote, lakini nitajiamulia mwenyewe,” alisema James Muturi, ambaye ni mkazi wa Thika.

Wengi wa wananchi waliohojiwa walikiri ya kwamba bado hawajaisoma kwa makini lakini wanatarajia kufanya hivyo bila kusomewa na viongozi.