Maoni

MAONI: Polisi wasitumiwe kuvuruga haki ya Wakenya kuandamana


RIPOTI za tafiti za kura ya maoni zimekuwa zikimkweza waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki kuwa kidedea katika uchapakazi ikilinganishwa na mawaziri wengine wa serikali ya Kenya Kwanza.

Ripoti iliyotolewa na shirika la InfoTrak wiki iliyopita, kwa mfano, ilisema Prof Kindiki anaongoza kwa uchapa kazi kwa asilimia 60.

Utafiti huo ulisema kuwa idadi kubwa ya Wakenya walioshiriki walisema kuwa Prof Kindiki ndiye waziri anayeongoza kwa kutatua changamoto zinazokumbwa raia.

Ripoti hiyo ilimweka waziri wa Michezo Ababu Namwamba katika nafasi ya pili kwa asilimia 52.

Inaonekana watu wanaoshiriki katika tafiti hizo wanavutiwa na hatua ya waziri Kindiki kuangaziwa na vyombo vya habari akiwa katika maeneo ya nchi akijaribu kutatua changamoto za usalama.

Wasichokijua wengi ni kwamba kuna uwezekano kwamba kuna mawaziri wasioonekana katika vyombo vya habari mara kwa mara ambao ni wachapakazi kuliko Prof Kindiki.

Ukweli ni kwamba Prof Kindiki amekuwa akitumia maafisa wa polisi kukandamiza haki ya Wakenya kuandamana kinyume cha matakwa ya Katiba.

Kifungu cha 37 cha Katiba kinawapa Wakenya haki ya kutangamana, kukusanyika na kuandamana almradi wasiwe na silaha. Lakini tumekuwa tukiona serikali ikitumia nguvu kutawanya waandamanaji wasiokuwa na silaha.

Mwaka jana, Prof Kindiki alionya vikali wanasiasa ambao wangethubutu kuongoza maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2023 kwa kisingizio kwamba maandamano hayo yangesababisha uharibifu wa mali.

Serikali imekuwa ikitumia kisingizio cha uharibifu wa mali kukandamiza haki ya kuandamana humu nchini. Kisingizio hiki ni sawa na msemo kwamba: fisi akitaka kula wanawe huanza kwa kuwasingizia kwamba wana harufu ya mbuzi.

Mapema mwaka huu, polisi walitumia nguvu kutawanya madaktari waliokuwa wakiandamana kutetea haki yao; hali iliyosababisha kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Dkt Davji Atellah.

Katika kulinda haki ya Wakenya kuandamana, Prof Kindiki anapata alama ya asilimia 10.

Tayari tumeona maafisa wa polisi wakikabiliana na waandamanaji wanaopinga Mswada wa Fedha wa 2024 kwa kuwarushia vitoa machozi.

Kwa mujibu wa wataalamu, Mswada wa Fedha wa 2024, unakandamiza raia na haufai kwani utasababisha gharama ya maisha kwenda juu.

Hivyo basi, maafisa wa polisi hawafai kutatiza maandamano ya Wakenya kabla na baada ya kupitishwa kwa mswada huo. Maandamano ndiyo sauti ya Wakenya viongozi waliowachagua wanapowasaliti.