Maoni

Maoni: Ujana si moshi machoni pa ‘M7’ wa Uganda

Na DOUGLAS MUTUA August 31st, 2024 2 min read

KIJANA maarufu zaidi wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni…. Naam, hujakosea, huyo hasa.

Usimwite mzee, anajiona kijana wa jana. Tofauti? Haijui, anaamini ujana wake hauishi, eti atasalia kijana milele.

Usimchezee ‘Msaba’, tulivyomwita siku zetu za utotoni tulipomwona kama shujaa wetu.

Leo hii anaudhi, ila hatujali sana maudhi yake kwa kuwa tukitaka kusema mambo ya hovyo, hata kutukana kidogo, tunamsimsingizia.

Ama unataka kuniambia hujakutana na nukuu bandia zinazohusishwa naye mitandaoni, ila ukichunguza unapata zimetungwa?

Alichukua nafasi hiyo ya kusingiziwa baada ya mzee kijana mwingine wa Afrika, Robert Mugabe wa Zimbabwe, kwenda mbele za haki.

Huyo naye tumemsingizia kila kitu wakati wa hayati yake; ikiwa kusingizia ni dhambi, huenda tulimkosha maovu yote aliyotenda duniani siku akichukulia kuwa Afrika ni mali yake, sote wengine wapangaji tu.

Nimekwambia ‘Msaba’ anajiona kijana kwa kuwa akili zake zinafanya kazi sawasawa hata kuwazidi vijana wengi wasiotimu umri wa miaka 35.

Hata hivyo, unakumbuka kweli amekonga anapoanza kutukana, au, sahihi zaidi, tuseme tu kuteleza ulimi, kama mzee mwingine wa kawaida, hasa Mwafrika.

Juzi amesema kuna mtoto fulani nchini Kenya kwa jina Babu ambaye anashirikiana na maadui zake wa kisiasa nchini Uganda, lakini hajali sana vitendo vyake kwa kuwa Babu hafanyi hivyo kwa niaba ya Babaman.

Nilijiuliza mara moja: ‘Msaba’ alijuaje Babu haingilii masuala ya ndani ya Uganda kwa niaba ya Babaman? Mbona ‘Msaba’ anakuwa muungwana na rafiki kwa Babaman kiasi hicho?

Samahani ikiwa nafikiria mambo yangu, lakini ni heri nikosee na niwe salama. Kwangu mimi ni vigumu kumwamini ‘Msaba’.

Ni mzee mjanja ambaye, hata akikalia kigoda chake mjini Entebbe, huona mbali kuliko sisi sote tunaomdharau na kusema astaafu na kupeleka ng’ombe wake malishoni.

Labda hata hana nia njema, anamuunga mkono Babaman kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) ili Waganda wakichoka naye, au akichoka nao, awanie wadhifa huo wa AUC Babaman akimaliza mihula yake miwili.

Usiniambie eti Babaman ni mzee sana, na kwamba mwishoni mwa muhula wake wa pili ‘Msaba’ atakuwa kikongwe cha kujiinamia.

‘Msaba’ mwenyewe hajioni hivyo. Hapendi tabia ya Wakenya kustaafu wakiwa bado vijana. Haikosi anashangaa mstaaafu wa Ichaweri aliondoka Ikulu akafanye nini kijijini. Anajiuliza Ouru anatumnia muda wake mwingi kufanya nini nje ya Ikulu.

Nadhani mpango wa ‘Msaba’ ni kutawala Uganda mpaka achoke. Usiniambie amechoka, akichoka atasema mwenyewe.

Na akichoka? Amwachie urais mwanawe, Mkuu wa Majeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ajaribu kuonyesha Afrika na dunia kwa jumla kuwa uzee si ugonjwa kwa kutamani kuongoza AUC.

Labda haya ni mambo yangu, lakini situmii akili kama vyombo vya wageni, iko kazini saa 24 kwa siku. Afrika hakuna kinachonishtua.

Ukitaka kuepuka ugonjwa wa moyo na msongo wa mawazo, kubali kwamba chochote kinaweza kutokea.

[email protected]