Maoni

MAONI: Umaskini pekee usiwe kigezo cha kuamua wa kupokea basari

February 21st, 2024 2 min read

NA JURGEN NAMBEKA

HATUA ya Gavana wa Lamu, Issa Timammy kutangaza kuwaondoa wanafunzi 700 kutoka kwa mpango wa ufadhili wa masomo, basari iliibua hisia kali miongoni mwa wakazi wa Lamu, ambao walisema watoto wengi huenda wasikamilishe masomo yao.

Kulingana nao, hatua hiyo ingewafanya watoto wa kike kuolewa na wale wa kiume kugeukia mihadarati. Kwa mujibu wa Bw Timammy, wanafunzi hao walipaswa kuhakikisha wanapata angalau alama ya C ili waendelee kupokea ufadhili wa masomo.

Licha ya pendekezo hili kuwakwaza wengi na wakazi wakiwemo viongozi , ni kweli kuwa ufadhili mara nyingine unapewa wanaojituma.

Kuzaliwa katika familia isiyojiweza ama yenye mapato ya chini, siyo kigezo cha pekee cha wanafunzi kupewa ufadhili wa masomo.

Mara nyingi kila mfadhili anapojitolea kutoa msaada, yeye hutaka matokeo ya mwanafunzi anayefadhiliwa, yaonyeshe juhudi na asiwe afuja pesa zake.

Malalamishi ya wakazi yanaonyesha “kustahili” kwa wanafunzi hao kupewa ufadhili kwa sababu wanafaa.

Hata katika ufadhili mwingi duniani unaotolewa, wanaofaidika hupaswa kulipia ufadhili huo kwa bidii yao. Endapo watakosa kutia bidii au kukosa nidhamu hatimaye wao hutupwa nje ya mfumo huo.

Kwa mujibu wa Bw Timammy, wanafunzi wanaopata ufadhili huwa wamechaguliwa kwa sababu ya kuandikisha matokeo mazuri katika mitihani ya KCPE.

Kwa hivyo, hakuona haja ya serikali kufadhili mwanafunzi ambaye pindi apoingia shuleni alipunguza bidii na kuandikisha matokeo duni.

Ni wazi kuwa mfumo huu ukitiliwa mkazo, kuna uwezekano wa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kutoka kaunti hiyo na Pwani kwa ujumla kuongezeka.

Hakuna haja ya kuweka hela nyingi za umma kwa mwanafunzi ambaye atachukulia ufadhili kama ibada na kuzembea shuleni.

Gavana anapasa kutafuta njia ya kuonya wanafunzi hao kabla ya ufadhili kuondolewa.

Katika miradi mingi ya ufadhili ya elimu, wanafunzi wanaofeli licha ya kuwa katika miradi ya ufadhili huandikiwa barua na nakala kupewa wazazi au walezi wao, kuwaeleza kuwa endapo hawataongeza juhudi, ufadhili wao utasitishwa.

Kwa ushirikiano na walimu wakuu wa shule zilizo na wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali ya kaunti, afisi ya gavana inaweza kuwafuatilia wanafunzi na hata kutoa onyo kila wanapozembea na kuwapokonya wanaochukulia ufadhli kama haki yao.