Maoni

MAONI: Watanzania wajue, kushindana na Wakenya ni sawa na kushindana na ndovu kunya!

Na DOUGLAS MUTUA August 16th, 2024 4 min read

HIVI majuzi nimemuudhi mtu nilipomwambia kuwa Tanzania ya sasa ni Kenya ya miaka ya themanini. Alikereka ajabu kwa kuwa yeye ni Mtanzania.

Si kidemokrasia; si kielimu; si kimtizamo wa maisha kwa ujumla, Wakenya wamewapiku Watanzania kwa kila kitu.

Na tatizo kuu ni kwamba Watanzania wengi wanaipigania kwa meno na kucha hali yao hiyo ya kubaki nyuma, hawataki kukosolewa. Nimewaza na kuwazua, ila mpaka sasa sijajua kwa nini taifa zima linaridhika na mambo kuliendea visivyo.

Kwa sasa, ikiwa wewe ni Mkenya, puuza ukweli kwamba hivi majuzi Bunge la Tanzania limetumia kikao kizima kujadili jinsi wafanyabiashara wa Kenya wanavyopaswa kufukuzwa kutoka Tanzania.

Naam, kufukuzwa hasa, kana kwamba wao si wawekezaji. Unashangaa, katika enzi hii ya kila taifa kujibidisha kukuza uchumi wake, Tanzania inakuaje kwa kuwafukuza wawekezaji?

Visa vingi vimeripotiwa ambapo Wakenya na pesa zao wamekwenda kubarizi Tanzania, wakalala kwenye hoteli nzuri tu na kutumia mafedha yao humo, kabla ya kuondoka wanaitiwa maofisa wa uhamiaji kwa tuhuma za ‘wapo Wakenya hapa, na nia yao haieleweki’.

Mwishowe, inabainika kuwa Wakenya hao ni majirani wa kawaida tu waliounda pesa zao, wakaamua ‘kurudishia mwili shukrani’ kwa kutalii Tanzania, nchi yenye mbuga za wanyama za kupendeza, na fukwe safi za baharini. Haturuhusiwi kuchangia makuzi ya uchumi wa jirani?

Mbona nchi hiyo isiige mfano wa Kenya, ambayo imewaruhusu mabwanyenye wa Kisomali kuwekeza mabilioni katika sehemu na nyanja mbalimbali, sikwambii wamejengewa na ofisi ya kulipia ushuru mtaani Eastleigh, Nairobi!

Hilo la Tanzania kufukuza wawekezaji linawahusu wageni, majirani zao Wakenya, ila kuna mengine mengi yanayowahusu Watanzania wenyewe ambayo kwa hakika unajiuliza iwapo hayawakeri, ya kuwakera ni yepi?

Bila shaka ukitagusana na Watanzania watakwambia kuwa Kenya tunakumbwa na njaa kila mwaka. Watakukumbusha pia kwamba Wakenya tunahasimiana kikabila; unafiki wao hauwaruhusu kukufichulia kuwa urithi mkubwa walioachiwa na marehemu Rais John Magufuli ni ukabila.

Wanayokunyamazisha kwayo ni kweli, lakini wapuuze tu kwa sababu kuwepo njaa na ukabila nchini Kenya si jawabu la masaibu yanayowasibu.

Na shibe yao haijawasaidia. Mtu haishi kwa mkate pekee!

Tanzania inaishi miaka ya themanini ambapo watetezi wa demokrasia nchini Kenya walikamatwa na kuzuiliwa kiholela bila kufikishwa mahakamani.

Huu ni mwaka 2024, lakini Tanzania bado inawakamata viongozi wakuu wa upinzani rasmi kwa kudiriki kuhudhuria mikutano wa hadhara.

Hivi majuzi polisi walimkamata mwanasiasa matata, Bw Tundu Lissu, ambaye aliwania urais dhidi ya Magufuli na kuibuka wa pili mnamo mwaka 2020.

Mwingine aliyekamatwa ni kinara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho cha pili kwa ukubwa baada ya kinachotawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw Freeman Mbowe na viongozi wengine wengi.

Wote hao walishikwa wakiwa njiani kwenda kuhudhuria mkutano wa vijana mkoani Mbeya. Ajabu, Watanzania waliketi kitako tu na kutazama viongozi wao wakidhulumiwa haki yao ya kutangamana, yaani kunyanyaswa bila makosa yoyote.

Serikali ilichukua hatua hiyo kwa kuogopa kwamba viongozi hao wangewapa vijana mshawasha wa kushiriki siasa kikamilifu yapata mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu ujao, ambao unamkosesha usingizi Rais Samia Suluhu Hassan.

Ukitaka kujua Kenya tumepiga hatua kubwa kidemokrasia, hebu tafakari serikali ya Dkt William Ruto ikiwatia kizuizini vigogo wa siasa zetu kama Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na wengineo.

Kenya inaweza kukalika kweli? Si kila kitu kitasimama mpaka watoke jela? Hata tusiende huko, hilo haliwezi kutokea! Dkt Ruto mwenyewe – na hata watangulizi wake – anajua kuna mambo ambayo si ya kuchezewa. ‘Salamu’ za kizazi kichanga kiitwacho Gen Z zilimkumbusha hulka yetu.

Kila Mkenya anajua ana haki ya kimsingi ya kutangamana, na yuko radhi kufa akiitetea, ndiyo maana hata tukipigwa na polisi hatusikii, wanaishia kusalimu amri na kuishi nasi tulivyo.

Wakenya tumezoea kumkosoa na hata kumtukana na kumpa majina ya msimbo rais wetu kila anapofanya maamuzi yasiyofaa na kugeuka king’ang’anizi asiyesikia. Kadri anavyoshupaa shingo ndivyo tunavyompa shinikizo mkumbo mmoja mpaka anakubali kutusikiliza.

Anayethubutu hilo Tanzania huishia jela; wanaharakati wengi wako gerezani. Kuwatia ndani wasio na hatia ni mbinu iliyotumiwa na aliyekuwa dikteta wa Kenya, marehemu Daniel Moi, kuwanyamazisha wapiganiaji haki kwa miaka 24. Moyo wa mapambano ungali nasi, haufi.

Mnamo mwezi Juni mwaka huu, kijana kwa jina Shedrack Yusuph Chaula, 24, aliadhibiwa kwa kifungo cha miaka miwili gerezani kwa kumkosoa Bi Suluhu.

Kosa lake ni kwamba alijirekodi video na kuipakia mtandaoni akiteta kuhusu uzembe wa Bi Suluhu katika kushughulikia suala la ushoga nchini Tanzania, kisha akachoma moto picha ya rais huyo.

Na inaonekana kijana wa watu alikiaminia alichokisema kwa kuwa hukumu hiyo ilipotolewa, aliiambia mahakama kwamba hajuti, yuko tayari kutumikia adhabu hiyo kikamilifu.

Moto uliounguza picha ya Bi Suluhu ulikwisha kuzimika, lakini naamini tendo la kijana huyo liliwasha moto mkubwa zaidi nyoyoni za Watanzania ambao wanachukizwa na mambo yanavyokwenda katika nchi yao, lakini hawawezi kuthubutu kusema chochote wasifie na kuozea jela!

Ikiwa Tanzania inataka kukua na kufikia kiwango cha uchumi wa kati kikweli, si madai tu, inapaswa kujua kuwa hata wajasiriamali wanaotoka Afrika ni wawekezaji pia.

Kampuni za ujenzi zinazomilikiwa na Wasomali, Waganda, Wanigeria na raia wa kwingineko Afrika zimetekeleza miradi mikubwa na muhimu kwa ufanisi wa kupigiwa mfano nchini Kenya.

Wawekezaji wazito kutoka Kenya pia wapo kote Afrika, sikwambii baadhi yao wanatekeleza miradi mikuu ya kijeshi kwenye mataifa ya watu na hawachukuliwi kama washukiwa wa jinai.

Si siri kwamba Watanzania wamejaa nchini Kenya, ambako wanafanya biashara za kila aina – kama vile kuuza nguo kuukuu na kutumiwa na wajanja wetu kama walemavu bandia ili kuomba hela mitaani – na, kama mke wa mlevi, tunawavumilia tu.

Watanzania watafaidika zaidi wakipanua mawazo na kukubali ushindani, katika nyanja zote. Waganda walitambua hilo wakajifunza nasi, sasa wanatushinda mbio ndefu. Tunawahongera, hatuwachukii.

Tukiwekeza Tanzania tunaajiri Watanzania, tunalipa ushuru Tanzania, tunaikuza Tanzania. Na Afrika Mashariki inafurahia, hivyo Tanzania iache unoko wa ukewenza.

Kwa sasa, Tanzania kushindana na Kenya ni sawa na binadamu kushindana na ndovu kunya!

[email protected]