• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 11:56 AM
CECIL ODONGO: Cheche za Malala zitabomoa UDA na kufifisha umaarufu

CECIL ODONGO: Cheche za Malala zitabomoa UDA na kufifisha umaarufu

NA CECIL ODONGO

KATIBU Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Cleophas Malala, anaonekana kulewa mamlaka kiasi cha kutoa matamshi ambayo yanaonyesha wazi kwamba utawala wa sasa haumakinikii umoja wa nchi.

Kauli tata ambazo katibu huyo mpya ameanza kutoa huenda zikachangia kupunguza umaarufu wa UDA inayoongozwa na Rais William Ruto.

Siku chache tu baada ya kukabidhiwa wadhifa huo na Seneta Veronica Maina, Bw Malala amekuwa kote kote katika vyombo vya habari akitupa cheche kali kwa upinzani na hata vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza.

Akiwa mjini Kisumu mwishoni mwa wiki jana, aliropoka maneno yaliyotokeza kama aliyelewa mamlaka na mtumwa wa mwanasiasa fulani.

Malala alidai kwamba watu wa eneo la Nyanza wataimarisha nafasi zao za kupata ajira au kuingia katika jeshi, idara ya magereza na shirika la misitu iwapo watajisajili kuwa wanachama wa UDA.

Kwa mujibu wa seneta huyo wa zamani wa Kakamega, kuhitimu kwa alama za juu na kupata shahada hakutoshi kumpa mtu kutoka ngome ya upinzani kazi, ila lazima awe mwanachama wa UDA.

Je, wanachama wote wa UDA, ambao wanasiasa wa chama hicho wamedai ni zaidi ya milioni saba, wana ajira?

Sheria ya vyama vya kisiasa inaruhusu Mkenya kuwa katika chama kimoja pekee cha kisiasa.

Ina maana huwezi kuwa katika ODM na UDA wakati mmoja.

Kulingana na Bw Malala, kijana aliyehitimu ila yupo ODM ana nafasi finyu ya kupata ajira ikilinganishwa na yule aliye UDA.

Kama ni hivyo, Kenya ina kibarua kufanikisha umoja wa nchi ambao ulikuwa maono ya waanzilishi wa taifa.

Ikumbukwe kuwa waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini miaka ya 90, walitaka kuwe na uhuru wa kujieleza na pia taifa linalozingatia demokrasia.

Huwezi kubagua watu katika utoaji ajira eti kwa sababu wanaegemea mrengo fulani wa kisiasa.

Kama kigezo cha uaminifu na uanachama wa vyama kitatumika wakati wa usajili wa makurutu nchini, basi ni wazi kuwa ngome za UDA ndizo zitanufaika.

Malala afahamu kuwa maeneo ya upinzani anayoyalenga yaliunga Raila Odinga hata katika tawala zilizopita wala si wakati huu wa serikali ya Kenya Kwanza pekee.

Changamoto zinazowakabili Wakenya ni zile zile – mtu awe upinzani au serikalini.

Kuna maeneo ya upinzani ambayo yamepiga hatua kimaendeleo kuliko ngome zingine za UDA.

Kama katibu mkuu wa chama kilicho uongozini, kazi ya Malala ni kufuatilia utendakazi wa viongozi wake na kuhakikisha ahadi zote walizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni wanatimiza.

  • Tags

You can share this post!

Wahadhiri wapata ujuzi zaidi wa masuala ya kiteknolojia...

Kocha wa Thika Queens afichua mipango msimu huu katika KWPL

T L